Saturday, June 21, 2014

Deni la Taifa Limevunja Rekodi, Unatishia Uchumi, Usalama wa Nchi, Dalili ya Kufilisika

Hotuba ya Mpango wa Maendeleo kama ilivyosomwa na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Ofisi ya Rais- Uratibu na Uhusiano, Esther Matiko, Hotuba Bajeti Mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kama ilivyosomwa na Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia na docs nyingine inayoonesha utoafuti kati ya Bajeti ya Kambi ya Upinzani na Bajeti ya Serikali ya CCM.

Kwa Kfiupi:

 DENI LA TAIFA
1.   Mheshimiwa Spika, Deni la Taifa limeongezeka kwa kasi kubwa sana, hali ambayo inatishia ustawi wa taifa kama halitasimamiwa kwa umakini na haraka. Hotuba ya Waziri wa Fedha inaonesha kwamba hadi kufikia Machi 2014, Deni la Taifa lilifikia shilingi trilioni 30.563 ikilinganishwa na shilingi trilioni 23.674 la Machi 2013. Hili ni ongezeko la takribani trilioni 7 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 29 kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.
 
2.   Mheshimiwa Spika, hili ongezeko la mikopo ya takribani shilingi trilioni 7 kwa mwaka mmoja tu, halijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu. Ongezeko hili la takribani trilioni 7 ni sawa na bajeti nzima (full budget) ya mwaka 2008/9 ambayo ilikuwa ni shilingi trilioni 6.839. Ikumbukwe kuwa mwaka 2008/9 ni miaka mitano tu iliyopita.  Ukopaji wa namna hii unatishia uchumi  na usalama wa nchi.
 
3.   Mheshimiwa Spika,   kwa  mujibu wa ripoti za Benki Kuu na hotuba za bajeti za miaka iliyopita za Mawaziri wa Fedha, deni la Taifa limeongezeka kwa kasi kutoka shilingi trilioni 9.3 mwaka 2007/8 hadi shilingi trilioni 30.6 mwaka 2013/14. Hii ni wazi kuwa deni liliongezeka kwa kiasi cha shilingi trilioni 21.3. Serikali imelipa shilingi trilioni 4 na kufanya fedha zilizokopwa kuwa jumla ya shilingi trilioni 25.3 katika kipindi hicho cha miaka saba tu. Huu ni ukopaji hatarishi kwa uchumi wa taifa letu.
 
4.   Mheshimiwa Spika,  licha ya deni hili kuwa hatarishi kwa uchumi wa Taifa, Serikali bado inatajaria kuongeza deni hilo kwa kukopa shilingi trilioni 4.3 kama ilivyoainishwa katika bajeti ya mwaka 2014/15.
 
5.   Mheshimiwa Spika, Serikali imeonesha kushindwa kulipa deni hilo kwa kutumia vyanzo vyake vya mapato, badala yake imekuwa ikikopa ili kulipa deni. Mfano hotuba ya bajeti ya mwaka 2014/15 imeonesha kuwa  katika shilingi trilioni 1.8 zilizokopwa katika soko la ndani, zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zilitumika kulipa madeni ya hati fungani wakati shilingi trilioni 0.69 tu ziliwekwa kwenye miradi ya maendeleo.  Hiki ni kiashiria cha karibu sana kwa serikali kufilisika. Kukopa mikopo ya kibiashara yenye riba kubwa ili kulipa mikopo yenye riba ndogo au kwa uendeshaji wa kawaida wa serikali au taasisi zake ni kiashiria cha kutosha kuainisha maamuzi yasiyo na uelewa wa kawaida sana wa utawala na usimamizi wa fedha. (basic business and economic sense). Mikopo ya kibiashara hutafutwa kwa matumizi ya uwekezaji wenye lengo la uzalishaji.
 
6.   Mheshimiwa Spika, katika uchumi unaokuwa kwa wastani wa asilimia kati 6.5 na 7 kwa mwaka, ni vigumu sana kuweza kulipa deni la Taifa linalokua kwa wastani wa asilimia kati ya 15 na 30 kwa mwaka. Bila kuwa na vyanzo vipya vya mapato  au kusamehewa deni hili itakuwa vigumu sana kuweza kulipa deni hilo kikamilifu. Hii ni kwa sababu uwiano wa ukuaji wa uchumi hauendani na kasi ya ukuaji wa deni hata kidogo. Pamoja na upungufu wote huu, Serikali imeendelea kujitapa kuwa inakopesheka, na hivyo kuashiria kutokuwepo na hofu yeyote ya kukopa huku holela.
 
7.   Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi ni kuwa sehemu kubwa  ya mikopo hii inakopwa katika soko la ndani. Hali hii imekuwa ikileta ushindani mkubwa kwa wananchi na wajasiriamali wanaotaka kukopa ili kukuza mitaji. Hali hii hufanya riba za mabenki kushindwa kushuka na hivyo kuwaathiri wakopaji na uchumi wa nchi kwa ujumla. Kwa maneno mengine, serikali imekuwa inazuia wajasiriamali wasikope kwa riba za bei nafuu, hivyo kufanya baadhi ya wanaokopa kwa riba zilizopo, ambazo ni kubwa kufilisiwa. Hali hii hurudisha biashara nyuma na inainyima serikali fursa ya kukuza uchumi na kukusanya mapato zaidi.
 
8.   Mheshimiwa Spika, mataifa mengi duniani yanakopa na yana madeni makubwa. Suala la msingi la kutofautisha nchi  moja na nyingine ni kasi ya kukua kwa deni husika na matumizi ya mkopo huo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inauliza na kutaka majibu kutoka kwa Serikali matumizi ya fedha zilizokopwa na nchi yetu ndani ya miaka 7 ni yapi na yameleta maendeleo kiasi gani kwa Taifa ( value for money).

No comments: