Friday, June 20, 2014

Rais Kikwete Akusudia Kushika Chaki Tena

Opening of the National Defence College in Dar es Salaam in 2012
Rais Kikwete Akusudia Kushika Chaki Tena
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa anakusudia kurejea darasani kushika tena chaki kwa kuwa mhadhiri kwenye Chuo cha Taifa cha Ulinzi – National Defence College (NDC) cha Dar Es Salaam.
Rais Kikwete amelieleza hilo mchana wa leo, Ijumaa, Juni 20, 2014, wakati alipotoa Mhadhara (Lecture) kuhusu Usalama wa Taifa (The Security of the Nation) mbele ya wanafunzi wa Chuo hicho kilichoko Kunduchi, Dar Es salaam.
Rais Kikwete amewaambia wanafunzi wa kozi ya pili ya Chuo hicho kutoka nchini na nchi za jirani za Uganda, Kenya na Rwanda: “Najisikia mwenye raha sana kuweza kurudi darasani kutoa mhadhara huu. Tukio hili linanikumbusha enzi zangu katika Chuo cha Kijeshi cha Monduli (TMA). Ni matarajio yangu pia kuwa nitaweza kurudi kuwa mhadhiri katika Chuo hiki baada ya kukamilisha kazi yangu ya sasa.”
Rais Kikwete ambaye alizungumza kwa kiasi cha saa mbili, alianza mhadhara wake baada ya kupata maelezo kuhusu maendeleo ya Chuo hicho na baadaye akajibu maswali ya wanafunzi ambao walimwuuliza kuhusu mambo mbali mbali yanayohusiana na usalama wa nchi.
NDC kilianzishwa rasmi Septemba 2, mwaka 2012 na Chuo hicho kilizinduliwa Rais na Rais Kikwete Septemba 10, mwaka huo huo, 2012 wakati alipotembelea Chuo hicho kwa mara ya kwanza kufuatia juhudi kubwa za uongozi wake kuhakikisha kuwa chuo cha namna hiyo na cha aina yake kinaanzishwa nchini. Rais pia alifungua kozi ya kwanza ya Chuo hicho.
Kundi la wanafunzi wa kwanza kwenye Chuo hicho lilimaliza mafunzo yake Julai 23, mwaka 2013 na sasa chuo hicho kinaendesha kozi ya pili yenye wanafunzi 30. Chuo hicho tayari kimepata usajili kamili wa NECTA ambako kina uwezo wa kutoa shahada ya uzamili katika masomo ya Strategic Studies.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU
DAR ES SALAAM
20 Juni, 2014

No comments: