Friday, May 20, 2011

Mtabiri Maarufu Sheikh Yahya Hussein Afariki Dunia!

(Pichani Hayati Sheikh Yahya Hussein)

Wadau, waTanzania wote tunafahamu umaarufu wa Sheikh Yahya Hussein katika mambo ya kutabiri yatakayotokea. Leo kuna habari kuna amefariki dunia. Lakini kifo chake imezua maneno!

Mungu Ailaze roho yake mahala pema peoponi. Amin.

********************************************************************
Kutoka Gazeti la NIPASHE:

Siku chache baada ya mtabiri mashuhuri wa Afrika Mashariki na Kati, Sheikh Yahaya Hussein wa Dar es Salaam kutangaza katika vyombo vya habari kuwa mwana CCM atakayejitokeza kuchuana na Rais Jakaya Kikwete katika kinyang’anyiro cha kugombea urais mwaka huu, atakufa ghafla, Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Glory of Christ Ubungo ametoa masharti matatu kwa mtabiri huyo vinginevyo naye atakufa ghafla.

Katika mahubiri kanisani hapo jana, Mchungaji Kiongozi, Gwajima alisema demokrasia ya Tanzania imo hatarini endapo mtu mmoja ataachiwa kuamua hatma ya taifa kinyume na mapenzi ya Mungu asiyekuwa na upendeleo kwa mtu yeyote.

“Baada ya kuendelea kutenda kazi zake zikiwa ni chukizo machoni mwa Mungu, leo ninatoa hukumu kutoka kwa Bwana, nanyi nyote mtachuja kuwa ni upi utabiri wa kweli kati ya Sheikh Yahaya na Mungu. Ninamwagiza Sheikh Yahaya afanye mambo matatu la sivyo naye atakufa ghafla kama alivyowatishia Watanzania wenzake,” alisema.

Sharti la kwanza alisema ni Sheikh Yahaya kwenda katika kanisa hilo la Glory of Christ na kuonana na mchungaji Gwajima yeye mwenyewe ili amwongoze kwa sala ya toba, kisha ampokee Yesu katika maisha yake.

Sharti la pili, Sheikh Yahaya ameamriwa kuanzia sasa aachane na utabiri wake ambao kwa miaka mingi alisema umewaumiza watu wengine wasiokuwa na hatia na kuwafaidisha wengine wachache kwa njia za giza.

Na sharti la tatu, Sheikh Yahaya ametakiwa, baada ya kuokoka, arudi katika vyombo vya habari kwa nguvu ileile aliyoitumia kutangaza utabiri wake wa mtu kufa ghafla na sasa awatangazie Watanzania mabaya yake yote aliyokwishayafanya kwa watu wa taifa hili hadi siku ya mwisho alipolazimika kuokoka.

Akifafanua juu ya masharti hayo, Mchungaji Gwajima alisema kimsingi yeye anamkubali Rais Jakaya Kikwete kuwa kiongozi wa taifa hili ila kinachomkera ni Sheikh Yahaya kuwatisha watu wengine wasitumie haki yao ya msingi katika kuikuza demokrasia hapa nchini.

Alipohojiwa kwa njia ya simu, Sheikh Yahaya ambaye alisema yuko nje ya jiji la Dar es Salaam kwa siku ya jana, alisema katika kipindi cha miaka 40 ya utabiri wake umekuwa sahihi siku zote na umaarufu wake ni wa kimataifa.

“Kamwe sitakwenda katika kanisa hilo, pia siko tayari kufuata sharti hata moja kutoka kwa mchungaji huyo.
Nimeanza utabiri kabla ya yeye kuwa shemasi wa kanisa hivyo endapo nitakufa najua ni siku zangu zimefikia mwisho wala si vinginevyo,” Sheikh Yahaya alisema.
Akitoa mifano ya utabiri wake ambao aliosisitiza kuwa sahihi mara zote, alitabiri msiba wa Mzee Rashidi Mfaume Kawawa kwa maelezo kwamba taifa litapata msiba mkubwa. Pia alisema aliwahi kutabiri kifo cha kiongozi mashuhuri ambaye kifo chake kingewakutanisha watu wa mataifa mbalimbali, dini, rangi na vyama mbalimbali vya siasa na kwamba kiongozi huyo alikuwa hayati Mwalimu Nyerere.

“Je, sikutabiri kuwa ndani ya CCM utazuka mtafaruku na kusababisha ufa ndani ya chama hicho kitu ambacho ninyi waandishi mmekishuhudia hivi karibuni?

Mimi siwezi kuongea kashfa yoyote dhidi ya mchungaji huyo bali ninachosema akipenda apeleke malalamiko yake Ikulu, kwani nako huko wapo watu wa kumjibu waliozishuhudia kazi zangu kwa miaka yote,” alitamba Sheikh Yahaya.

Alisema alitarajia kiongozi huyo wa kanisa aempe mwaliko rasmi waonane mahali popote siyo hapo kanisani ili waelezane masula ya nyota kwa undani badala ya ‘kumtisha’.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Rest in Peace Sheikh Yahya Hussein! Sikutegemea kama unaweza kufa!