Wednesday, May 25, 2011

Mauji Tarime - Maiti Zadhalilishwa!

Yaani sikutegemea kusikia habari za ajabu kama hizi kutoka Tanzania. Kwanza watu wameuawa, pili bado tunaibiwa urithi wetu na mzungu! Sasa maiti wanadhalilishwa! Yaani tunakwenda wapi jamani?

Habari Kutoka WAVUTI.Com

Umekuwepo mkanganyiko mkubwa baina ya wafiwa, Serikali na wanaharakati, kufuatia mauaji ya watu kadhaa waliouawa na Askari Polisi kwa kupigwa risasi wakituhumiwa kutaka kupora Mgodi wa dhahabu wa African Barrick North uliopo katika eneo la Nyamongo, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, Tanzania.

Mkanganyiko huo wa ama maiti wazikwe au la ili kupisha uchunguzi, umesababisha mtafaruku ambao umewaacha maiti hao wakiwa wametelekezwa mitaani, vile vile, baadhi ya wanaharakati na viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, wamekamatwa kuhusiana na tukio hili.

Washitakiwa walikana kosa na kurejeshwa rumande kwa 'sababu za kiusalama' kufuatia ombi la Mwendesha mashtaka alkiiomba mahakama kutokutoa dhamana kwa watuhumiwa kwa madai kuwa dhamana hiyo ingeweza kuhatarisha amani na kuchochea ndugu wa marehemu kutoendelea na taratibu za mazishi.

Polisi pia iliwashikilia kwa muda na kuwahoji Mbunge Ester Matiku (Viti Maalumu-CHADEMA), John Heche na waandishi wa habari wanne Mabere Makubi (Channel TEN), Anthony Mayunga (Mwananchi), Berdina Nyakeke (The Citizen) na Anna Mroso (Nipashe) kuhusiana na tuhuma hizo za uchochezi.

Polisi yatoa sababu ya kuchukua maiti

Imearifiwa kuwa miili ya marehemu iliwekwa katika majeneza bila kuvikwa nguo zozote wala sanda na kupelekwa nyumbani kwa wahusika lakini wanakijiji walikataa kupokea maiti hao wakitaka polisi kuirejesha miili hiyo hospitalini ili ichukuliwe upya na kuzikwa kwa heshima na mila za Wakurya. Ndipo ilipotelekezwa barabarani, “Mimi nimefiwa na mtoto wangu Emmanuel Magige, jana tuliambiwa asubuhi ndio tutachukua miili ya watu wetu tukazike sasa tumeamka tunaambiwa eti polisi walichukua marehemu wamekwenda kuwatupa porini na sisi tuko hapa Tarime...” - mzee Magige Ghati, baba wa mmoja wa marehemu.

Baada ya waandishi wa habari kusikia taarifa hiyo, walikwenda ili kushuhudia na ndipo walipokamatwa.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi Tarime/Rorya, Costantine Massawe, alisema kuwa walichukua miili ya maiti baada ya wafiwa kuwaomba msaada wa kuwapelekea miili hiyo katika vijiji vyao.

Alisema, baada ya baadhi ya wafiwa kuchukua miili hiyo juzi na kuisafirisha kwao, wafuasi wa CHADEMA waliwafuata hadi Nyakunguru na walipofika huko, waliishawishi familia ya Magige kuuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka Polisi kwa nia ya wanahabari waliofuatana nao kuupiga picha ili kuonesha taswira kuwa Polisi imetelekeza miili hiyo ili kupotosha jamii na kujenga chuki kwa Jeshi hilo na wananchi wa Tarime

source: WAVUTI.COM

1 comment:

Anonymous said...

Sasa haya ni mambo gani mnaleta siasa mpaka kwenye misiba??badilikeni ndugu zangu hasa wa chadema mana mnaonesha uroho wa madaraka tu kwa kuleta hizi vurugu......hawa chadema wanafikiri wapo juu ya sheria ndio mana hata wabunge wao bungeni wanaropoka eti ..''fungeni milango tupigane'' msituharibie nchi yetu wanafiki wakubwa.....