Tuesday, May 24, 2011

Shairi - Tuacheni Jamani - Mauaji Tarime!

TUACHENI JAMANI!

Tuacheni jamani!
Polisi tuacheni
Serikali tuacheni
Yenu kazi tayari
Iliyobaki ni yetu!

Sisi ndio wafiwa Tarime
Walioporwa uhai wa ndugu
Uhai wa vijana wabichi

Tuacheni sisi
Sisi ndio wafiwa
Kazi yenu tayari
Ile ya kuua
Kazi yetu yaja:
Kulia, kulaani,
kuomboleza na kuzika.

Tuacheni tulie
Hata kulia mwazuia?
Tuacheni tunune
Hata kununa mwazima?
Tuacheni tuzike
Hata kuzika mkwara mwaweka?

Serikali na polisi
Msingeua tusingelia
Msingeua tusingenuna
Msingeua tusingezika
Tuacheni, tuacheni.

Lenu mmemaliza
Kuua mkilinda nyang'au
Mkilinda mporaji
Mnyakuzi wa mali ya Tarime
Mali ya Tanzania
Tuacheni
Kutuchefua acheni.

Mwizi mkubwa mwalinda
Mwenye mali mwaua
Kwa ujira gani mwatenda
Unyama usio mithili
Mijitu yachota utajiri
Kwao yajenga mbingu
Ninyi: Kwenu
Hapa kwenu, miayo yatanda
Zaidiyo mwaua wanenu
Wezi wa nje kulinda. Tuacheni!

Mmemaliza kezi yenu
Kuua, kulinda nyang'au
Sasa amri mwatoa:
Lia hivi, nuna hivi...Ebo!
Na udikiteta una mipaka.

Tuache tunune kwa ngeli yetu
Tuache tujute kwa mazoea yetu
Tuache!

Tuache tulie machozi yetu
Yatiririke mashavuni mwetu
Yaloanishe vifua vyetu
Yaondoe hasira zetu

Tuache tukunje wafu wetu
Tubebe kwa njia zetu
Tusindikize kwa ngeli zetu
Tuzike mashambani kwetu
Tuache!

Acha Tarime wazike
Wazike kwa mila zao
Kwa uzito wa uchungu wao
Kwa kina cha chuki yao
Kwa wingi wa hasira zao.
Tuacheni jamani!

Hata baada ya kuua
Wakilinda wezi
Wanataka tulie roborobo
Tunune nusunusu
Tuchukie roborobo
Tukasirike nusunusu
Tulaani roborobo
Tushutumu nusunusu
Tuzike juujuu
Au nasi tuuawe moja kwa moja.
Tuacheni jamani.

Tarime zikeni.
Tundu Lissu zika
Marando Nyaucho zika
Zikeni vijana wenu
Kwa ngeli yenu
Kwa ngeli ya wakazi
Wanavyotaka
Wanavyojisikia

Tuacheni jamani
Polisi kaa mbali
Serikali jitengeni
Kazi mliyojipa tayari
Ilobaki ni ya walioumia
Waliopoteza
Tuacheni jamani!

Imetungwa na Ndimara Tegambwage

No comments: