Friday, May 27, 2011

Wanafunzi Wamwua Mwalimu Wao Iringa!!

Duh! Yaani nimesoma kwa mshangao mkubwa habari za hao akina dada kumwua mwalimu wao! Kisa alitaka kumbaka moja wao. Ubakaji ni mambo mazito, mimi ningempa adhabu ya kukatwa dhakari, lakini kuua hapana! Inaninikubusha ile sinema ya The Women of Brewster Place, yule dada shoga anabakwa na kundi la wahuni halafu anapata kichaa na kumwua kwa kumpiga kichwana mara kadhaa, baba aliyekuja kumsaidia.

Mungu ailaze roho ya Dr. Mafingo, mahala pema mbinguni. Amen. Hao wasichana watafute wakili mzuri la siyo watasota huko jela miaka mingi.

****************************************************************
Kutoka Gazeti la NIPASHE

Wanafunzi wa Kike Wamuua Mwalimu
By Godfrey Mushi
27th May 2011

Wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi cha Bulongwa kilichoko Wilaya ya Makete mkoani Iringa, wamemuua kwa kumshambulia kichwani mkufunzi wa chuo hicho, Dk. Jumbe Mafingo, kwa madai ya kupinga jaribio lake la kutaka kumbaka mwanafunzi mwenzao.

Taarifa za awali za makachero wa polisi zilieleza kuwa mkufunzi huyo aliuawa baada ya kutuhumiwa kwamba alitaka kumdhalilisha kijinsia mwanafunzi wa kike, Jean Laison Mwakabuta kwa kutaka kumbaka.

Tukio hilo la kuuawa kinyama kwa mkufunzi huyo ambaye ni mwalimu wa nidhamu chuoni hapo, lilitokea juzi usiku nyumbani kwake mjini hapa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla, Dk. Mafingo alifikwa na umauti baada ya mwanafunzi huyo kuamua kwenda nyumbani kwake usiku ili kumkabidhi maelezo yake ya kimaandishi kuhusu sababu zilizomfanya alale nje ya chuo.

Ilielezwa kuwa muda mfupi baada ya kuingia kwenye nyumba ya mwalimu huyo, mwanafunzi huyo alianza kupiga kelele kuwa anabakwa.

Alisema kufuatia kelele hizo, wanachuo wengine waliamka katika vyumba vyao na kwenda hadi eneo la tukio na kuanza kumshambulia kichwani mkufunzi huyo hadi kumuua.

Kamanda Mangalla alisema Dk. Mafingo aliuawa kwa kushambuliwa na kitu kizito kichwani.

“Huyu Jean Laison Mwakabuta, aliambiwa na Dk. Mafingo ambaye ni mwalimu wa nidhamu chuoni hapo, aandike maelezo ya maandishi kwa sababu gani alilala nje ya chuo,...baada ya kuandika maelezo hayo, aliamua kuyapeleka nyumbani kwa mkufunzi huyo usiku, sasa baada ya kugonga mlango na hatimaye akaruhusiwa kuingia, alianza kupiga kelele kwamba anabakwa…na ndipo wanafunzi wenzake waliposikia kelele wakaamka na kukimbilia eneo hilo na kumshambulia mkufunzi huyo hadi kufa,” alisema Kamanda Mangalla.

Ilidaiwa kuwa siku moja kabla ya tukio hilo, uongozi wa chuo hicho cha Bulongwa ulitoa ridhaa kwa wanachuo wote kwenda kutembea nje ya chuo kwa lengo la kuwapunguzia msongo wa mawazo ya masomo na Jean Laison Mwakabuta hakurejea chuoni hadi siku iliyofuata.

Kamanda Mangalla, alisema wanachuo wanne akiwamo mwanafunzi Jean, wametiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo.

SOURCE: NIPASHE

7 comments:

Anonymous said...

Haya maelezo ya wanafunzi naona hayajitoshelezi yanaacha maswali mengi kuliko majibu, sasa huyu binti kilichomfanya kupeleka barua usiku nyumbani kwa Mwl wake ni nini? siku mzima alikuwa wapi? Pili hayo makelele walisikia hao wanafunzi wanne tu? halafu anapoishi mwl hakuna nyumba ya jirani yaani majirani yake hawakusikia hayo makelele ni hao wanafunzi wanne tena wakiwa mabwenini!! Ubakaji ni mbaya ila kuua mtu ni kubaya zaid.
B

Anonymous said...

Mmmh! kwa kweli sasa wanafunzi wa kike mnaharibu sana tena sana! hapo ni kifungo cha maisha tu tena watatoa huduma gerezani kwa shule waliyoisoma.Kwanza kwenda usiku kwa mwl ulitarajia nini hasa kutoka kwake kama sio kumtia majaribuni mwl wako!Na waliohusika huenda walijua mipango yote kabla ya tukio,wafuatiliwe na wapewe adhabu kali sana ili iwe fundisho kwa wengine.

Anonymous said...

Ni hao wanne tu waliosikia kelele za huyo dada?

Anonymous said...

Mhhh. Huyo mdada anamatatizo makubwa nanin alimwambia apeleke hizo taarifa nyumbani tena usiku? hakuiona ofisi? kwa mtizamo wangu, huyu mdada alikuwa amepanga kummuua Dr.Kama taarifa inavyosema kwamba Dr aligongwa na kitu kizito, huyu mdada alipofuguliwa mlango alimshushia marehemu nondo ukizingatia Dr alikuwa hakujiandaa kwa lolote. Mdada alipomaliza kazi yake alipiga kelele kwamba anabakwa ili kufuta ushahidi.

Anonymous said...

maelezo hayaleti maana. Kwakweli kumtoa mtu roho inakatazwa katika misahafu na vitabu vya dini zote.

Huyo dada amakatumiliwa au kuna jingine ndani ya saga hii yote.

Maskini familia ya huyo marehemu, kwanza wanauguza donda la kupotolewa na mpenzi ndugu yaho na tena kazi ya kusafisha jina na sifa yake, kwani jamii itamhukumu hata kabla wahusika kufanya kazi yao ya kubaini ukweli.

Anonymous said...

Big up Jean! wanawake simameni imara, hivi visa vya aina hii kila aliesoma shule za Bongo anavijua wakuu wanatumia nyadhfa zao kunyanyasa kijinsia wanawake, imefikia mahala wanawake nao wamesimama imara, iwe mfano kwa nyie wengine, FUNGENI ZIPU

Anonymous said...

UKIJIHESHIMU NA WEWE UTAHESHIMIWA, SAA MBILI USIKU UNAAGIZA BARUA ILETWE NYUMBANI?????