Wednesday, September 16, 2009

Mwakilishi Wetu Big Brother Africa 4

Kutoka ippmedia.com


Hatimaye mwakilishi wa Tanzania katika shindano la Big Brother Africa mwaka huu amejulikana na tayari ameshaanza kufanya vitu vyake.

Mbongo huyo ambaye sasa ameondoa dhana potofu ya awali kwa baadhi ya watu kuwa msanii Steven Kanumba ndiye aliyekuwa mwakilishi wa Tanzania kwa mwaka huu, ni mrembo Elizaberth Gupta mwenye umri wa miaka 21.

Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Msemaji wa Kampuni ya Multichoice (Tanzania), ambaye kampuni yao hiyo yenye maskani yake Afrika Kusini ndiyo inayoendesha shindano hilo, Bi. Furaha Samalu, amesema tayari Elizaberth ameshatinga kwenye jumba la BBA nchini Afrika Kusini na kuanza vitu vyake.

Akawaomba Watanzania waendelee kumpa sapoti ili hatimaye aweze kufanya vyema, kwani ushindani wa mwaka huu ni mkali zaidi.

"Yuko fiti sana... naamini atafanya vizuri, lakini Watanzania tumuombee na kumuunga mkono ili kufikia azma hiyo," akasema Bi. Furaha.

Aidha, akigusia wasifu wa Elizaberth, Furaha amesema ni mwenye uelewa mpana na ana uwezo mkubwa wa kuzungumza Kiingereza, lugha ambayo ndiyo inayotumika kwenye jumba hilo.

"Hana tatizo la lugha... ana uwezo mkubwa sana na ndiyo maana akapata fursa hii ya aina yake," akaongeza.

Uthibitisho huo wa uwezo wa kuzungumza lugha ya Kiingereza alio nao Elizaberth unaondoa shaka kuwa pengine, naye atakwazika kiasi na kutaniwa pindi akirejea nyumbani, kama ilivyo sasa ambapo baadhi ya watu walikuwa wakitumiana vimeseji vya utani, vikidai kuwa eti, Mbongo akiwa kwenye jumba hilo la BBA atashindwa kuzungumza vyema na kuwaambia wenzie kwa lugha 'broken' kuwa: "I am closing... I will open in ze evening!"

Waliotunga utani huo, walikuwa wanamaanisha kuwa: "Nimefunga (swaumu ya Ramadhani), nitafungulia jioni)."

Utani huo uliosambaa wiki iliyopita kupitia vimeseji vya simu na kwenye mitandao ya internet, ulitokana na ushiriki wa saa 24 wa msanii Kanumba, ambaye alikuwa mmoja wa mastaa wanne walioalikwa kwa ajili ya uzinduzi wa shindano hilo la BBA Revolution kwa mwaka huu.

Maelezo mengine kuhusu Elizaberth yanaonesha kuwa alizaliwa miaka 21 iliyopita na ni miongoni mwa warembo walioingia kwenye 10 bora ya fainali za kumsaka Mrembo wa Tanzania mwaka jana.

Ameingia kwenye shindano hilo akiwa na usongo mkubwa wa kuwa mshindi na kutwaa zawadi ya kitita cha dola za Kimarekani 200,000.

No comments: