Tuesday, September 22, 2009

Wananchi Msidanganywe na Mafisadi - TAMWA

Kutoka http://www.ippmedia.com/

Tamwa Yawaasa Wananchi Wasidanganywe na Mafisadi
Na Mwandishi wetu

22nd September 2009

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) kimewataka wananchi kuwachunguza kwa makini wagombea uongozi katika vitongoji, vijiji na mitaa ili kuepuka kuwachagua wala rushwa na mafisadi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Ananilea Nkya, alisema wagombea hao wasichaguliwe kwa kuwa ni adui wakubwa wa maendeleo.

"Wananchi wanapaswa kuwachunguza kwa makini watu wote watakaogombea uongozi katika vitongoji, vijiji na mitaa ili kuepuka kuwachagua wala rushwa na mafisadi ambao ni adui mkubwa wa maendeleo ya wananchi," alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jijini jana.

Alisema umuhimu wa wananchi kuwachunguza wagombea unatokana na ukweli kuwa matatizo mengi kwenye vitongoji, vijiji na mitaa yanatokana na baadhi ya wananchi kutotambua kwamba kura yao ndicho kitu muhimu wanachoweza kutumia kuwanyima uongozi wala rushwa na mafisadi.

Alisema ili uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika nchi nzima tarehe 25 mwezi ujao uweze kuweka madarakani watu ambao si wala rushwa na mafisadi ni muhimu wananchi wote watambue kuwa kipindi cha uchaguzi siyo lele mama, bali ni kipindi cha kutafakari kwa makini na kufunga mkanda ili kuepuka vishawishi vya watu wanaonunua uongozi kujinufaisha.

Alisema kutokana na baadhi ya wananchi kutokuwa makini wakati wa uchaguzi, katika miaka ya hivi karibuni uongozi wa umma umegeuzwa kuwa ni mradi wa wanaopata uongozi kujitajirisha badala ya kutumikia umma, hali ambayo inachangia kushamiri kwa kero za wananchi na umaskini miongoni mwa wanawake na wanaume wengi nchini.

"Wagombea wala rushwa na mafisadi huwa wanatumia mbinu kuwadanganya wapiga kura ili kushinda uchaguzi ikiwa ni pamoja na kuwatisha wananchi, kuwahonga vyakula, vinywaji, mavazi, simu, fedha au kuwapa ahadi za uongo.

"Wala rushwa na mafisadi wakishapata uongozi katika mitaa na vijiji, huzitumia ofisi hizo kwa manufaa yao binafsi zaidi hasa kujitajirisha kwa kuuza na kukodisha mali za mitaa na kuwatoza wananchi fedha wanapokuwa wanahitaji huduma ya kiongozi kwa ajili ya kutatua matatizo yao," alisema.

Alisema baadhi ya viongozi wala rushwa huwatoza wananchi fedha kati ya sh. 1,000 na sh. 5,000 bila kuwapatia risiti wanapohitaji kupata barua ya kuwatambulisha kama wakazi wa eneo husika au kama wanahitaji huduma ya kiongozi kutatuliwa matatizo binafsi yanayowakumba. Alisema Tamwa inaona kuwa viongozi wengine wala rushwa na mafisadi wamekuwa ndio chanzo cha serikali kulalamikiwa na wananchi kutokana na kuua miradi ambayo inaanzishwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Kwa mfano, alisema mwaka 1998 serikali ilijenga visima vya maji safi katika mitaa ya jiji la Dar es Saam ili kupeleka huduma hiyo karibu na wananchi, lakini katika baadhi ya mitaa viongozi waliochaguliwa na wananchi wamegeuza visima hivyo kuwa ni miradi yao binafsi ya kujipatia fedha na katika vingine katika mitaa kadhaa vimekufa kabisa kutokana na ubinafsi wa viongozi.

CHANZO: NIPASHE

No comments: