Thursday, July 31, 2008

Fujo kwenye Mazishi ya Wangwe - FFU waingilia!

Mdau Jacob Mugini kamletea Kaka Michuzi picha hizi sasa hivi kuonesha hali ilivyokuwa huko tarime kwenye mazishi ya hayti chacha wangwe. Juu ni meza kuu ambapo viongozi wa vyama vya siasa wakiwa wameketi, na chini ni baadhi ya waombolezaji. Duh, naona walikuwa roho juu juu hapo!

Na Mwandishi wa Globu ya Jamii, Tarime

Mazishi ya Mh. Chacha Wangwe, aliyekuwa Mbunge wa Tarime aliyefariki dunia kwa ajali ya gari majuzi huko Dodoma, yameshindwa kufanyika leo kijijini kwake Kamokorere baada ya kufumuka kwa vurugu kubwa ambapo wabunge na viongozi wa serikali na vyama vya siasa walohudhurian ilibidi watoke bomba kusalimisha maisha yao.

Vurugu hiyo ilianza dakika chache baada ya kuwasili kilioni hapo kwa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Mh. Freeman Mbowe, katika kijiji cha Kemokorere kiasi cha kilomita 20 hivi toka mjini Tarime.

Hali ilipokuwa mbaya, ilibidi Mh. Mbowe na viongozi wote waliohudhuria mazishini waondolewe kilioni chini ya ulinzi mkali wa FFU ukiongozwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Mara Afande Leberatus Barlow ambao walifanya kazi ya ziada kuepusha balaa.
Viongozi wengine waliohudhuria walikuwa ni pamoja na wenyeviti wa vyama vya upinzani Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Augustino Lyatonga Mrema (TLP), John Cheyo (UDP) James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Karatu Mh. Wilbroad Slaa pamoja na kiongozi wa upinzani bungeni, Mh. Hamad Rashid.

Wote hao walisindikizwa chini ya ulinzi mkali wa FFU kuondoka mahali hapo na kuelekea Musoma. Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Mh. Steven Wassira, na Manaibu Mawaziri ambao ni wabunge wa Kanda ya Ziwa, Dr. James Wanyacha na Gaudensia Kabaka nao ilibidi waondoke.
Ujumbe toka Kenya ulioongozwa na Dr Wilfred Machage ambaye ni mbunge wa jimbo la Kurya na pia Naibu Waziri katika serikali ya mseto ya Kenya pamoja na wakuu wa wilaya wawili nao walikuwepo na ilibidi waondoke kwa kuruka ukuta.

Tofauti na walivyoingia, itifaki haikuweza kufuata kama walipowasili wabunge 20 wakiongozwa na mbunge wa Bumburi Mh. William Lukindo vurugu hilo lilipoanza na ilibidi kila mmoja aondoke chini ya ulinzi mkali.

Maelfu ya waombolezaji, wengi wao wakiwa vijana waliobeba mabango yenye ujumbe mbalimbali unaohoji kifo cha Mh. Wangwe, walitawala hapo kilioni. Juhudi za Mkuu wa mkoa wa Mara Mh. Issa Machibya kuwatuliza hazikuzaa matunda.

Hata juhudi za kututuliza ghasia hizo za Wah. Zitto Kabwe na mmoja wa wanafamilia waandamizi kama vile Profesa Samwel Wangwe na Mkuu wa zamani wa Halmashauri ya Tarime Mh. Peter Wangwe pia hazikuambulia kitu.

Prof Wangwe aliwaambia waombolezaji hao wenye hasira kwamba familia ya Wangwe imeamua kumtafuta mtaalamu huru kuifanyia upya uchunguzi maiti ya hayati Chacha Wangwe ili kubaini alifariki kwa njia ipi.

Wengi ya waombolezaji wanatuhumu kwamba Mh. Wangwe hakufa kwa ajali ya gari. Mtu moja aliyekuwa na marehemu wakati wa ajali, Bw. Mallya, anahojiwa na polisi na uchunguzi wa kina unaendelea.
****************************************************
VURUGU zilizuka katika maziko ya Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, pichani,baada ya ndugu wa marehemu kugoma kuzika mwili wake wakidai hawajaridhika na maiti yao ambayo wanadai kuwa ina tundu la risasi.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alinusura kujeruhiwa kwa kumrushia mawe na wengine wakitaka kumkata kwa mapanga na aliokolewa kwa juhudi za ziada za polisi. Kabla ya tafrani hiyo kuzuka, ndugu wa marehemu waliigomea Serikali kumzika Mbunge huyo wakisema hadi uchunguzi mpya ufanyike waweze kujiridhisha kuhusu chanzo cha kifo hicho.

Ratiba ya maziko hayo ilikuwa ianze saa 7 mchana, lakini kuanzia saa tatu asubuhi, ukoo wa Wangwe ulikaa chini ya mwenyekiti wake Profesa Samwel Wangwe na kutoa uamuzi wa kutozikwa marehemu hadi daktari wa familia kutoka Dar es Salaam atakapofika na kuufanyia uchunguzi upya.

Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alifika katika msiba huo saa nane mchana akiwa amefuatana na viongozi wengine wa vyama vya siasa ndipo ghafla vijana walipotoa mabango yaliyokuwa yamebeba ujumbe mbalimbali wakipinga kuwa kifo cha Wangwe ni mipango ya Mungu.
“Hatutaki sura ya Mbowe tunataka mbunge wetu,” walisikika wakisema vijana hao ambao walikuwa tayari kutaka kumpiga mwenyekiti huyo wa Chadema, wakidai kuwa chama chake kimehusika katika kifo cha Wangwe,baadaye wengine walitoa mapanga na mikuki, hali iliyowalazimu polisi kumchukua Mbowe na kumwingiza ndani ya nyumba ambako walikuwa wamekaa wabunge wengine 20.

Kuona hivyo vijana wengine walianza kurusha mawe kuwaelekezea viongozi hao. Viongozi hao kuona hivyo walitimua mbio wakihofia maisha yao. Baadhi ya viongozi waliotimua mbio pamoja na Mbowe ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Salehe Ramadhan Feruzi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, Zitto Kabwe ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Mwenyekiti wa CCM Mkoani Mara, Makongoro Nyerere na Mjumbe wa NEC wa CCM wa mkoa wa Mara, Christopher Gachuma.

2 comments:

Anonymous said...

Mazito! Lakini halahala wabongo wameamka siku hizi! yale mambo ya kukaa kimya kama za enzi za Mwalimu zimepitwa na wakati!

Anonymous said...

Chemi punguza basi hizi habari kutok a kwa michuzi..Mara nyingi watu tunakuwa tushaziona kule kwa Michuzi.Jaribu kuwa original otherwise kama huna kitu cha kublog kaa kimya tu..sio lazima