Tuesday, July 01, 2008

Kuolewa siku hizi ni fasheni au kuondoa nuksi?

Mwandishi wa habari, Flora Wingia, anauliza na kuchambua swali nzito. Inafurahisha kweli kweli.

**********************************************
Kutoka ippmedia.com

Eti wanaoolewa siku hizi ni fasheni ya kuondoa nuksi?

2008-06-29


Na Anti Flora Wingia

Mpenzi msomaji, lipo jambo moja limenivutia kukumegea leo kuhusu ndoa za siku hizi. Huko tulikotoka kuolewa au kuoa lilikuwa ni tukio la baraka. Lakini siku hizi hali ikoje? Liko tukio moja nililosimuliwa kutoka huko Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo dada mmoja aliolewa siku ya Jumamosi, lakini siku mbili baadaye, yaani Jumanne akamwacha yule bwana na kutokomea kwa mwanaume mwingine. Kisa ni nini?

Msimulizi wa tukio hili anasema kuwa dada huyo japokuwa alikuwa na mchumba huyo waliyefunga naye ndoa, lakini hakuwa anampenda kwa dhati bali alikuwepo mwingine wa ubani, tena mume wa mtu aliyemzibua kimapenzi.

Kwa maelezo ya bibie eti mchumba yule hakumpenda ila alitaka afunge naye ndoa ili kuondoa nuksi na iwe kwenye kumbukumbu kwamba hata yeye aliwahi kuoewa kwa ndoa takatifu.

Mashuhuda wa harusi wa bibie huyo wanasema ndoa ilikuwa ya gharama kubwa na iliyofana lakini walishangazwa na taarifa kuwa ndoa imesambaratika na bibie kaenda kwa mshikaji wake ambaye ni mume wa mtu.

Inasemekana ndugu wa bwana harusi wamecharuka na kuapa kumrudisha bibi harusi kwa mumewe kwa gharama zozote zile. Na kwamba shugadadi huyo anayemzingua shemeji yao naye atakiona cha mtema kuni.

Hata hivyo, habari zingine zinadai kuwa bibie katu hatamrejea mumewe kwa kile alichodai, kwanza alitaka tu aolewe ndoa kuondoa nuksi na pili aliyemuoa hamridhishi kimapenzi.

Mpenzi msomaji, hayo ndiyo mambo na hakika maisha ndivyo yalivyo. Eti siku hizi kuolewa ni fasheni ya kuondoa nuksi. Wiki hii nilipata wasaa kusikiliza kipindi cha Longa mwanamume kwenye kituo cha televisheni cha ITV kikihusu baadhi ya kinamama kuwaachia watumishi wa nyumbani kufanya kazi ambazo zingepaswa kufanywa na wao.

Mfano, kumpokea baba arudipo kazini, kumwandalia baba chakula, kumwekea maji bafuni na hata kutandika kitanda. Eti kazi hizi zote alipaswa kuzifanya mama ili kumwepushia baba vishawishi vya kummezea mate housigeli. Nilipogusia jambo hili katika kikao Fulani na marafiki zangu juzi, mmoja akasema; ``Kinamama wengine wako katika nyumba zao tu kuweka rekodi kuwa wameolewa, lakini mapenzi hakuna``.

Mwingine akamdakia; ``wewe hujui ukiona hivyo ujue vituko vya mumewe vimemfika kooni. Pengine anapewa taarifa zake (mume) kuhusu nyendo zake za kihuni huko nje, au mume yule hamjali tena kama mwanzoni walipooana na kadhalika``.

Mwingine akapigilia msumari kwa kusema; ``katika nyumba nyingine ukiona mama hajali kumhudumia mumewe nyumbani, basi ujue anaye mshikaji nje ya ndoa anayemzingua hivyo mume si chochote. Bibie niliyemzungumzia mwanzoni mwa makala hii yeye hakutaka aone vurugu za ndoa ndio sababu akaamua kujiengua mapema na kwenda kumuegemea shugadadi wake.

Lakini swali ni je, haya ndiyo maisha tunayotaka? Hizi fasheni za maisha eti kuondoa nuksi zinatoka wapi? Je, huku ni kuondoa nuksi au ni kuharibiana kimaisha? Kwa ujumla yule mama anayempiga chenga mumewe ndani na kuchepuka kwa bwana wa pembeni, sidhani ana amani yoyote rohoni mwake.

Hali kadhalika yule bibie aliyemtosa mumewe wa ndoa muda mfupi na kukimbilia kwa mume wa mtu, bado atapata vikwazo na vishawishi vya kusaka mabwana wengine. Kama hukutosheka na mmoja ndio utatosheka na wanaume wengine lukuki?

Upo msemo mmoja wa mtaani usemao ``Nimezunguka bucha zote lakini nyama ni ile ile``. Hii ikimaanisha kuwa kile baadhi ya kinamama wanachokimbia kwenye nyumba zao ndio hicho hicho watakikuta kule waendako. Mpenzi msomaji, kinachotakiwa ni watu kuheshimu nyumba zao.

Mke au mume ulimtupia jicho mwenyewe, ukampenda sasa wamtilia shaka ya nini? Si maji uliyavulia nguo, sasa kwa nini uogope kuyaoga? Hakika Maisha Ndivyo Yalivyo. Kuolewa ni baraka toka kwa Mwenyezi Mungu siyo fasheni wala kuondoa nuksi kama baadhi yetu wanavyodai. Hata mababu zetu walifurahia sana ndoa na zilidumu tofauti na sasa ambapo tukio hilo linapewa uzito mdogo.

Siyo siri kuwa baadhi ya watu wanaoa au kuolewa lakini wanajenga au wanaendeleza mahusiano ya nje ya ndoa. Raha gani wanapata huko, wahusika wanajua. Faida gani wanapa ndio pamoja na maambukizi ya magonjwa hatari kama Ukimwi. Habari ndiyo hiyo.

Mpenzi msomaji, kwa leo naomba niishie hapa tukutane tena wiki ijayo. Ukiwa na maoni, ushauri usiache kunikandamizia kupitia email ifuatayo;

fwingia@yahoo.com. Wasalaam.

SOURCE: Nipashe

9 comments:

Anonymous said...

Jamaniiiiiiiiiii........yamenikuta binafsi mimi, lakini ni kwamba pamoja na kuondoa niksi, alikuwa na mipango ya kutaka afanikiwe kimaisha kupitia mgongo wangu......mapenzi hayakuwepo kabisa!!!!

Nililigundua mapema na namshukuru Mola kwa hilo, na sasa yupo Dar anahangaika na waume wa watu anashindwa kupata wake wapendane kwani kila mtu anasikia kuwa huyo aliwahi olea akaachika.

Na mimi nimempata mwenzangu anipendae na nimeoa na niko Ughaibuni tunaendesha maisha kwa raha na starehe.

Ukweli ni kwamba, kwa msichana au mwanamke kuachika au kusema kuachana na mumewe humuwekea doa ambalo kufutika kwake ni kugumu. Naomba niwakilishe tujadili katika kuendeleza mada iliyowekwa

Anonymous said...

mdau wa kwanza uko sahihi, ni dhambi sana kumdanganya mwenzio kuwa unampenda kumbe mnafiki,alafu unaamua kufunga nae ndoa ili mradi tu, mimi ni mkirsto na huwa naogopa sana mtu kuapa mbele za Mungu mtakuwa pamoja kwenye shida na raha alafu tena mmoja anatengua kiapo na kumsaliti mwenzio, nimeona wengi tu hamna alietengua kiapo kanisani akafunga ndoa na mtu mwingine alafu akafurahia maisha wengi huwa wanajuta wanakumbuka ndoa zao za kwanza. wadada tuache tabia mbovu kama hizi hazifai kwa jamii ndoa ni baraka kwa Mungu.
Ms Bennett

Anonymous said...

dada chemi asante kwa hii mada, binafsi inanigusa, mimi nina mchumba wangu tunapendana tumekuwa pamoja yapata miaka 2 sasa, mwaka jana mwezi wa 8 alipropose kutaka kunioa na kweli nampenda nilikubali na kuwambia baadhi ya ndugu zangu hata marafiki wanajua. kwa sasa mchumba ana matatizo makubwa ktk familia yake na ameona ni bora kuahirisha kufunga ndoa mwaka huu ili ajaribu kwanza kusolve problems za familia yao,na mimi nimekubali nitamsubiri tu hamna shida, basi kwa kuwa baadhi ya ndugu zangu na rafik wanajua jamaa alisha propose imekuwa nongwa hawaishi kuuliza maswali huyo jamaa vipi atakuwa anakuzingua tu na kupoteza mda rafik yangu anajaribu kusema anitafutie mwingine hata mdogo wangu ambae ameolewa alikuwa anachombeza eti kuna rafik wa mume wake anataka mchumba hivyo aniunganishe, yote nimekataa kwa sababu nampenda mchumba wangu na siwezi mwacha kwa kuwa ana matatizo hata hivyo nashukuru Mungu nina ujasiri. wadau nimeamua kutoa story yangu kama changamoto kwa wadada wenzangu wapo ambao wanaamua kuolewa kwa shinikizo la ndugu, rafik, wazazi,umri n.k lkn naweza sema kwamba mtu afanyae hivyo hayuko tayari kwa ndoa bali anaolewa kama fashion au kuridhisha tu ndugu na jamaa.mwishowe inakuwa shida baadae, ndoa ni kitu special toka kwa Mungu na inahitaji kumuomba sana Mungu kwenye swala la kumpata atakae kuwa mwenzi wa maisha.
linah

Anonymous said...

Hii mada si ya mchezo.Dunia inabadilika na inaendelea kubadilika.Sisi binadamu popote pale tuwapo twahitaji kubadilika pia. swala ni kubadilika kwa upande bora au mbaya.Mimi binafsi ndoa sio sherehe wala sio kutoa nuksi. Naamini kabisa kwa kileo kuwa ndoa ni maelewano kati ya watu wawili tu walioamua kuishi pamoja na kujenga kiota pamoja.Kwenda kanisani au kuangusha mnuso kabambe hiyo kwangu haina maana yoyote. Wengi wanadai kuwa kabla hujaamua uwe na fulani katika uhusiano huo basi yabidi kwanza mjuane kwa muda ili utafakari akufaa ama la. kwa kiasi ina maana lakini watu hubadilika baada ya muda na pia wakati huo wa kutafakariana wengi wetu huwa ni vigumu kujifumbua hasa hivyo kuficha baadhi ya tabia zao njema au mbaya.Kwa kiasi kumpata mwenza ambaye mtashibana huwa kama bahati tu.Kitu kingine ni kuwa waishio pamoja mbali na upendo wa kweli kati yao inabidi waweze kuelimishana,kusameheana,kusaidiana,kutokuwa na bwana na kitwana nk.Ndoa za zamani zilitawaliwa na udikteta na dharau, zilimchukulia mke kama mtumwa, mtekelezaji na mtu asiye na usemi-utmwa.Hivyo wengi walikuwa ni watekelezaji tu, mashine za kutotoa watoto na vihongo vya kazi na zaidi ilikuwa ni lazima kumyenyekea mwanaume. Ndoa nyingi ziliishi kwa woga na wala sio mapenzi.Siku za leo wanawake kiasi wana uhuru, usemi na kuamua.Wengi hawako tayari kuvumilia na huamua uhuru hata bila kufikiria. Hii pia ni kwa vijana wa leo.Kuachana hapo zamani kulikuwa ni jambo la aibu na pengine usipewe fursa tena ya kuoa, lakini leo ni kawaida tu na kila kitu nje nje.Jambo jingine hasa fikra zetu waafrika zinabidi zibadilike.Unyumba kuongelea hadharani ni tabuu,hatuwafundishi watoto wetu namna ya maisha. mfano msichana kujikinga kupata mimba.Sasa inapotokea mtoto kupata upeo wa kuangalia nje akakumbana na maendeleo ya kileo kama TV, INTERNET na MEDIA za kileo basi anachanganyikiwa na anapoamua kuiga kidogo chochote kile akionacho au kukisia anaibuka na madhara chungu nzima na anaharibu maisha. Zamani haya mambo hayakuwepo! Vijana wetu wa leo wanapenda kuiga maisha ya west bila kujua kuwa hawajaandaliwa kuishi maisha kama hayo matokeo ni simanzi.Hivyo nawashauri waafrika wenzangu kujaribu kutafuta na kujua chanzo cha madhara haya ndio kuyakabili na wala sio kulaumu huyu na yule. Naamini kwanza jamii zetu zinabidi kujiandaa KUBADILIKA NA KUJENGA JAMII KWA NAMNA TIFAUTI NA ZAMANI.
AHSANTENI

malisa

Anonymous said...

Mwanamke hafuati chakula, gari, nyumba bali mtu kama alivyo in oneness fresh and soul.

Anonymous said...

itakuwa vema sana kila mara ukitoa nakala za frola kwani zinaelimisha na kufundisha kwa kiasi kikubwa sana ktk maisha ya kila siku kwa walioolewa na wasioolewa!asante sana kwa ujumbe mzuri!
tafadhali dada che mponda tuma zaidi na zaidi nakala za huyu mama ktk blog yako.
its me E.Banzi

Anonymous said...

Mr E Banzi Frola ni nini?

malisa

Anonymous said...

Kweli tunayo safari ndefu. Cha ajabu ni kwamba habari za wanaume wanaowaacha wake zao mara baada ya kuwaoa haziandikwi kwa vile huchukuliwa kawaida na ni haki yake ila akifanya mwanamke huwa ni cha ajabu sana. Kwa huyu nakubali kuwa ana makosa kumwacha mwenzie amwoe then anamkimbia. But ni wanaume wangapi tunasikia wanawaacha wake zao? tena wengine hata kanisani au sehemu ya kufungia ndoa hawafiki kabisa je hao wako sahihi? Mbona Anti Flora hujawaleta hao nao wasulubishwe?

Nway kama hujampenda mtu ni bora uwe muwazi siku hizi hakuna cha kutoa nuksi wala nini alomwambia kuwa kutoolewa ni nuksi ni nani/ ni vile unavyoichukulia jamii kama unaiacha jamii ikuchagulie namna ya kuishi basi utaona ni nuksi kweli otherwise fuata matakwa yako uishi kwa amani ya moyo kuliko kuishi kama jamii itakavyo huku ukiugumia moyoni- Maisha yenyewe mafupi ishi upendavyo tena live life to the fullest

Anonymous said...

Biismilahi rwahmani rwahim.Daa kweli Mungu nimkubwa.mmnilikua napita thu nikisoma mambo ya dini,nikakutana na hii story alioandika dada huyu.Imebidi nisite nisome yote.

Kwakweli nimeshangazwa na maneno ya binti huyo. Napia nimesoma comment ya mwenzangu mmoja hapa kuelezea kua aligunduakua mumewe alimuoa ili kujipatia kutoka kwake kulikua hakuna mapenzi. Subhannallah.

Mimi naezaelezea kisa chakwangu. mm nimke wamtu imeolewa nanimuislam Alhamdhulillah.nilijuana na mume wangu akatoa posa nakunioa. ila kwakweli mm sina furaha kwenye ndoa yangu hatha Mungu anajua. mumewangu alianza kuzini nje kunikaripia hakua anaongea namm vizuri bila sababu. hadi ikafikia wakati kunionesha wazi kabisa kua anatembea na wanawake wengine nje. mm moyo wangu unaniuma sana ila kwadini yangu naendelea kumuomba Mungu ambadilishe. Kwamana niliolewa kimapenzi na kwamoyo wangu wote. ila niligundua kua mumewangu alinioa kwasababu yake hakua na penzi na mm.

eeh nduguzangu kumbukeni kua ndoa nidaraja ilioekwa na Mungu , mukivunja hio daraja hakuna daraja nyengine itakayokua yenye nguvu. Mungu akikupa pokea kwa imani na ushukuru. Dunia imekwisha watu wanacheza na ndoa zahaki. binadamu anaapa kwajina la Mwenyezi Mungu kupenda mke ama mume wake kwasida na furaha kumbe hapo hapo anajua anadanganya. astaghafurullah.

binadamu wengi wetu wamesahau dini nawanacheza na jina la Mungu. Wanachanganya Mungu na fashion. Sheitwani ametawala dunia. Tujue hili ili tubakie upande mwema. Chochote kinachotokea kibaya nicha sheitwani. Ila muamini Mungu ataogopewa na sheitwani.