Sunday, August 30, 2009

Maonyesho ya Filamu Hadharani Marufuku-Mkuchika

Naona wanapunguza milo ya watu! Yaani leo ndo wanarudisha Bodi ya Ukaguzi wa Filamu! Video na DVD zilivyozagaa nchini Bongo mbona watakuwa na kazi ngumu!

**********************************************************
Kutoka ippmedia.com

Na Mwandishi wetu

Serikali imepiga marufuku maonyesho yote ya filamu kwenye hadhara ya watu, majumba yasiyo rasmi, hoteli na maeneo ya baa bila kufuata masharti kwa mujibu wa Sheria.

Agizo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika, wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Ukaguzi wa Filamu nchini ambayo itakuwa na jukumu la kukagua na kusimamia maonyesho na shughuli za filamu nchini.

Alisema sehemu nyingi zinazotumiwa kuonyesha filamu hazina leseni halali za kuonyeshea na kuongeza kuwa sio salama kwa mali na afya za watu. “Nachukua fursa hii kutoa onyo kwa mtu yeyote atakayeonyesha filamu kwenye hadhara ya watu katika majumba yasiyo rasmi, vibanda, kumbi ndogondogo, hotelini, baa na katika vyombo vya usafiri waache mara moja,” alisisitiza.
Alifafanua kuwa sehemu nyingi zinazotumika kuonyeshea filamu sasa hazikidhi matakwa ya ujenzi wa kumbi za kuonyeshea filamu na ni kinyume cha sheria kwani nyingi zimekuwa chanzo cha maficho ya wahalifu, majambazi, biashara ya dawa za kulevya na kuchochea vitendo vya ngono kwa vijana.

Alisema athari nyingi tayari zimeshajitokeza katika jamii yetu na kuongeza kuwa filamu nyingi zimechangia kubomoa na kudunisha Utamaduni wa taifa letu na hata kuchangia kwa kiasi kikubwa kubomoa misingi ya amani , Upendo , Uadilifu, heshima, uaminifu na utu ambao ni utambulisho wa mtanzania jinsi ulivyokuwa umejijenga na kuenea katika jamii yetu.
Aidha alisema serikali iko makini kuhimiza na kusisitiza matumizi ya sanaa katika masuala mbalimbali ya maendeleo na kuvitambua , kuvikuza na kuviendeleza vipaji vya wasanii katika kukuza taaluma na fani ya filamu nchini.

Awali akizungumza kuhusu majukumu ya Bodi hiyo, alisema kuwa Bodi itakuwa na jukumu la kuweka misingi ya kuimarisha utaratibu wa usimamizi wa utengenezaji wa filamu na pia kutoa vibali vya kutengeneza filamu hapa nchini.

Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo Bi. Rose Sayore ameihakikishia serikali kuwa Bodi yake itafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kuwa kanuni, sheria , maadili na taratibu za uonyeshaji na utengenezaji wa filamu zinazingatiwa kwa maslahi ya watanzania na vizazi vijavyo.

2 comments:

MICHUZI BLOG said...

Hahahaaa we acha tu. halafu badala ya kushughulikia piracy ambapo TZ inaongoza Africa wanaleta za bodi ya ukaguzi. Halafu siku hizi watu wanaangalia mpira ligi ya uingereza kwenye groceries. sijui itakuwaje..

Anonymous said...

Yaani kweli watu hawana kazi. Hii bodi haitaweza kufanya kitu. Kazi yao itakuwa kuwa posho za vikao.