Tuesday, May 27, 2008

Serikali Inajikanganya - Kifo cha Dk. Ballali

Misa ya Kumwombea Mzee Ballali huko Washington D.C. (picha kutoka Michuzi Blog)

Wadau, lazima niseme kuwa bado kuna maswali mengi kuhusu kifo cha Mzee Ballali.

************************************************************
Kutoka ippmedia.com

Serikali inajikanganya kifo cha Ballali - Slaa

2008-05-27

Na Simon Mhina

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa, amesema hoja za Waziri wa Mambo ya Nje, Bw. Benard Membe kwamba serikali haihusiki na kifo cha Dk. Daudi Ballali, hazijaisaidia serikali, badala yake zimezidi kuleta mkanganyiko.

Alisema yeye pamoja na wapinzani wengine, walijenga hoja kwamba ni kwa nini wanaihusisha serikali na kifo hicho, tofauti na Bw. Membe ambaye amekanusha bila kujibu hoja zao na wala hakutoa maelezo ya msingi.
Dk. Slaa, ambaye pia ni Mbunge wa Karatu, alisema waziri huyo amezidisha kiwango cha wasiwasi walichonacho watanzania, pale aliposhindwa kutoa maelezo kwamba Dk. Ballali alikuwa amelazwa hospitali gani na ugonjwa gani.

Alisema hoja ya Bw. Membe kwamba wanaotoa tuhuma dhidi ya serikali wanafanya hivyo kwa hisia, haina msingi na inadhihirisha jinsi waziri huyo anavyobabaika. ``Yaani ugonjwa wa mtu mkubwa mwenye tuhuma nzito kama Ballali, umefichwa, kifo chake kimefichwa, mazishi yake yamefichwa, hata Maiti yake haikuonekana, halafu anasema tuhuma zetu ni hisia? Huu ni upotoshaji mkubwa na kuzidi kujikanganya,`` alisema.

Mbunge huyo alisema kitu ambacho kingeweza kuinasua serikali katika tuhuma hizo, ni Bw. Membe kutaja sehemu aliyokuwa amelezwa Dk. Ballali. ``Tangu lini hospitali ikawa ni sehemu ya siri, kwa nini hawataki kusema?`` Alihoji.

Alisema madai aliyotoa waziri huyo kwamba mwenye vielelezo toka kwa daktari vinavyoonyesha kwamba Dk. Ballali alikufa kwa sumu avitoe, au yanaonyesha kwamba kweli kifo cha Gavana huyo wa zamani wa BoT kilipangwa. ``Mtanzania wa kawaida atawezaje kumpata daktari aliyemtibu Ballali wakati hata hospitali alipokuwa amelazwa panafichwa?

Kumbe wameficha kwa makusudi ili Watanzania washindwe kupata vielelezo?`` Alihoji na kuongeza: ``Serikali haihitaji vielelezo, bali ndiyo iliyofanya njama za kuhakikisha hakuna kielelezo chochote ambacho kinahusiana na kifo hicho kinachoweza kupatikana.``

Alisema kama kweli serikali inasisitiza kwamba haihusiki, itaje hospitali ambayo Dk. Ballali alikuwa akitibiwa na ugonjwa uliomsibu. ``Bw. Membe anasema mwenye vielelezo apeleke? Kazi yake kama waziri wa Mambo ya Nje ni ipi hasa?
Yeye ndiye alitakiwa azungumze na Balozi wetu kule Marekani ili aeleze habari za ugonjwa na baadaye kifo chake, kama mtu mkubwa kama Ballali anaweza kufikwa na kifo nchi za nje bila watu kujua, sembuse mtu wa kawaida?`` Alihoji.

Dk. Slaa alisema ili serikali ijisafishe, ni vizuri ikasema ni kwa nini hata hapa mjini, matanga ya marehemu huyo yalikuwa ya siri na majirani walikatazwa kuingia huku waandishi wa habari wakifukuzwa.

``Tunataka iundwe tume huru ya kuchunguza kifo hicho, kwa vile hadi sasa serikali haijatoa maelezo yanayojitosheleza. Tunataka tume kwa vile pesa za EPA bado ziko mikononi mwa mafisadi, ambao huenda ni marafiki wakubwa wa serikali,`` alisema.

3 comments:

Anonymous said...

Hivi kuna uhakika gani kuwa maiti ya Ballali imo kwenye hilo jeneza? Na hii ni funeral yake kweli mbona sioni waswahili?

Anonymous said...

REST IN PEACE. Let us remember the good he did when he was with IMF.

Anonymous said...

ballal bado hajarest in piece, bado anarest duniani, siku akifa watasema kafa mtoto wa ballal, mie najua alipo ballal, njooni niwaonyeshe!!