Monday, April 23, 2012

Kiingereza ni Kasumba!


Kufundishia Kiingereza nchini: Ni Kasumba tu Inayodumaza Elimu!

• Angalia Saa yako, unahesabu Saa kwa Kiswahili, lakini lazima utakuwa umeirekebisha isomeke kwa Kiingereza!

Na Saidi Nguba

Rais wa Kwanza wa Afrika Kusini huru, Nelson R. Mandela, aliwahi kusema katika nukuu zake nyingi za busara, kwa Kiingereza:“If you talk to a man in a language he understands, that goes to his head. If you talk to him in his language, that goes to his heart.” Kwa tafsiri yangu, ya Kiswahili: “Ukizungumza na mtu neno katika lugha anayoielewa, linamuingia kichwani. Lakini ukizungumza naye katika lugha yake, linamuingia moyoni mwake”.

Mbunge, Profesa Kulikoyela Kanalwanda Kahigi, ambaye ni mtaalamu wa lugha, akizungumza katika mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, bungeni mjini Dodoma Agosti mwaka 2011 alisema: “Lugha ni nguzo ya msingi ya kujenga uzalendo.

Vinginevyo utajengaje uzalendo kwa kutumia lugha ya kukopa ya kigeni?”.

Profesa Kahigi aliongeza: “Tunawafundishia vijana wetu kwa Kiingereza.

Je, tunawapa maarifa vijana wetu au tunawafurahisha mabwana zetu?”.

Hii ndiyo hali ilivyo nchini Tanzania, tuna kasumba ya Kiingereza, lugha ya kigeni na lugha ya kikoloni. Mpaka sasa, miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, uamuzi haujafanywa wa kuitumia Lugha hii adhimu ya Kiswahili kufundishia nchini katika ngazi zote, pamoja na kuwa lugha hiyo ina vigezo vyote vya kukidhi kazi hiyo. Hii haina maana kukipuuza Kiingereza, ambacho watu wengine hapa nchini wanakiita kuwa ni “Kiswahili cha Dunia”. Ni vizuri Kiswahili kifundishwe vizuri, kitumike kufundishia na Kiingereza pia kifundishwe vizuri kama lugha na liwe ni somo la lazima kwa kila mwanafunzi kuanzia darasa la kwanza, hadi Sekondari, ili wanafunzi wote, wakifika kidato cha nne, kwa mfano, wazungumze na kuandika lugha hiyo kwa ufasaha mkubwa.

Kasumba imefikia kuona jambo hili kuwa ni kitu cha kawaida. Kwa mfano, ukimuuliza mtumiaji wa Kiswahili, je, sasa saa ngapi? Atakujibu, sasa ni saa 6. Lakini mwambie aangalie alivyorekebisha saa yake. Utaona mshale, badala ya kuwa katika sita, uko kwenye namba 12, kama vile walivyozoea Waingereza, kwa mfumo wao wa kujua wakati. Saa 6 ya mchana, kwa Kiswahili, Kiingereza siyo “Six o’clock” ni “Twelve o’clock”!

Kiingereza ni Lugha siyo Elimu

Swali la kujiuliza: Je ni kwa nini basi tunaendelea na kasumba hii ya kukipa kipaumbele Kiingereza na kupata kigugumizi cha kukitumia Kiswahili kufundishia katika ngazi zote?

Ubishi unaoenea kwa kasi ni kuwa Kiingereza ni “Lugha ya Kimataifa” na kwamba kwa kufundishia, vijana wetu watakuwa na elimu inayolingana kimataifa. Pili, kwa vile hakuna vitabu vya kutosha vya Kiswahili, ukilinganisha na vya Kiingereza, kufundishia Kiswahili, ni tatizo.

Sababu zote hizi zinamfurahisha zaidi Mwingereza tu.

Ukweli ni kwamba Kiingereza ni lugha tu na mtu anaweza akajifunza, na kwa utaalamu wa kisasa wa kufundisha lugha na nyenzo zilizopo, hata kwa miezi mitatu mtu anaweza akakielewa na kuzungumza. Lugha siyo elimu, isipokuwa ni chombo cha kusaidia kutolea elimu. Elimu ni uwezo mkubwa wa kuelewa na kugundua mambo, ili hayo unayoyaelewa na kuyagundua yatakusaidia kuleta mageuzi katika maisha yako na ya binadamu wengine, kutoka kiwango fulani na kwenda kiwango cha juu zaidi chenye kuleta manufaa na tija. Ili elimu nayo itolewe kwa vizuri zaidi ni lazima lugha ya kufundishia iwe ile ambayo anayefundisha na anayefundishwa wote wanaifahamu vizuri. Pili, hakuna vitabu vya Kiswahili nchini kwa sababu havina soko. Mara uamuzi wa kufundishia Kiswahili utakapochukuliwa, basi vitabu vya Kiswahili vitakuwa biashara kubwa na vitaanzishwa hata “viwanda” vya kufyatua vitabu vya elimu mbalimbali kutoka lugha za kigeni na kuwa vya Kiswahili.

Wataalamu Wamekwishathibitisha

Uwezo wa Kiswahili kufundishia ili hatimaye elimu ikue kwa kiwango kikubwa nchini na kujenga taifa la kujitegemea badala ya kuendelea kuwategemea wengine kwa kila kitu, siyo mahitaji ya kisiasa, bali ni jambo linalowezekana na lililothibitishwa na wanataaluma wa elimu na wa lugha pia.

Profesa John Kiango, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wakati anamkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuzindua Taasisi mpya ya Kiswahili ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Julai 26, 2009, alisema: “Nikiwa mtaalamu wa lugha, napenda nichukue nafasi hii, kukuhakikishia kuwa Kiswahili kinaweza, na kikipewa nafasi kitaleta mageuzi ya kitaalamu na kiugunduzi nchini.”

Anaongeza:“Tafiti zimebaini kuwa nchi zote zilizo na ugunduzi asilia ambao siyo ule wa kuiga ni zile zinazotumia lugha zao. Nchi zinazotumia lugha za kigeni katika kutolea elimu zimebaki kuwa watumiaji wa teknolojia zilizogunduliwa mahali pengine, teknolojia ambazo tunauziwa kwa bei mbaya sana.”

Hatutaki tu kuuona ukweli. Kwa mfano, ukimuandaa mtaalamu wa Kilimo hadi anapata shahada, akija kuwa Bwana shamba kijijini, je elimu yake atawapatia wale wakulima kule vijijini kwa lugha gani? Kiingereza, alichojifundishia au kwa lugha ambayo walengwa wanaielewa? Kwa vile madhumuni ya elimu ni kwa watakaobahatika kuipata wawagawie maarifa na huduma wengine, kwa nini sasa tunalazimika hapa hapa nchini ambako tuna lugha yetu, kuifundisha elimu hiyo kwa lugha ya kigeni na ya kikoloni? Kama elimu utaipata kutoka China, ni dhahiri lazima kujifunza kwa Kichina.

Katika kitabu “Focus on fresh data on the Language of Instruction debate in Tanzania and South Africa” kilichoandikwa na Brigit Brock- Utne, Zubeida Desai na Martha Qorro, mwaka 2006, ikiwa ni sehemu ya matokeo ya tafiti za LOITASA (Language of Instruction in Tanzania and South Africa) ambayo ni Mradi wa NUFU (The Norwegian Programme for Development Research and Education) ulioanza mwaka 2001 na unaomalizika mwishoni mwa mwaka 2011, imebainishwa jinsi lugha ya Kiingereza ilivyokuwa tatizo katika ufundishaji kwenye shule za Sekondari nchini Tanzania.

Utafiti wa LOITASA ulifanywa katika shule mbili za Sekondari kwa kutumia utaratibu wa kufundishia somo la Baiolojia – darasa moja kwa Kiingereza na darasa jingine kwa Kiswahili. Kwa mujibu wa kitabu hicho, katika darasa lililokuwa linafundishiwa Kiingereza, wanafunzi walionekana kutochangamka na hawakuelewa kilichokuwa kinaendelea, wakati lile la Kiswahili, wanafunzi walikuwa wanachangia kwa uelewa wa hali ya juu na ukawepo mjadala wenye tija baina ya mwalimu na wanafunzi.

Tume ya Rais ya Elimu, iliyojulikana kuwa Tume ya Makweta (mwanasiasa na mwanataluma mashuhuri nchini) ilitoa mapendekezo ya kutaka Kiswahili kitumike katika ngazi zote, hatua kwa hatua, kuanzia kidato cha kwanza mwaka 1985 na Chuo Kikuu kuanzia mwaka 1992. Mapendekezo hayo mpaka sasa hayajatekelezwa.

Mapema tangu mwaka 1953, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), lilitoa azimio lililosema, pamoja na mambo mengine, ni vema hasa kwa elimu ya msingi kwa watoto wadogo, kuwafundisha kwa lugha wanazozielewa vizuri na hasa lugha za mama zao.

Sasa, kama wataalamu wamekwishamaliza kazi yao na kuthibitisha kuwa Kiswahili ni lugha inayojitosheleza kwa msamiati karibu katika kila fani, mbona Kiswahili hakitumiki nchini katika kufundishia, hasa elimu ya juu? Kwa nini?

Jibu la uhakika ni kwanza, matokeo na athari ya kutawaliwa na Waingereza na hivyo kupandikiza ndani ya akili zetu hali ya kutojiamini wenyewe, kuanzia katika lugha na hata katika maeneo mengine. Kazi yetu ni kuwategemea wengine, wa nje tu. Pili, kasumba tu ya kawaida kwamba Kiingereza ndiyo elimu na tatu ni kusita kuchukua uamuzi.

Sera; Dira, Hazitekelezwi

Sera ya Elimu ya Mwaka 1995 nchini inasema kuwa Lugha ya Kufundishia ni Kiswahili na Kiingereza. Sera hiyo inafanyiwa mapitio, lakini katika maandiko ya awali ya marekebisho yanayopendekezwa, haionekani kwamba uamuzi unafanywa wa kukitumia Kiswahili katika ngazi zote.

Kwa mfumo wa sasa nchini, kuanzia shule ya awali hadi darasa la saba, lugha ya kufundishia ni Kiswahili, lakini kuanzia kidato cha kwanza hadi kwenye vyuo, lugha ni Kiingereza. Ingawa ukweli ni kwamba hata kwenye vyuo, mwalimu akiona haeleweki kwenye ukumbi wa mhadhara, huwa anabadilisha lugha na anatumia Kiswahili na mara mambo yanabadilika na kwenda vizuri.

Katika Sera imetamkwa rasmi kuwa: “Serikali itakuza elimu ya awali ya watoto wenye umri wa miaka 0-6. Elimu hii itahakikisha kudumishwa kwa maadili yetu kiutamaduni”. Lakini hali halisi ya sasa, ni tofauti na tamko la Sera. Siku hizi kuna shule za binafsi nyingi zilizochipukia zinazofundisha kwa Kiingereza, ziitwazo kwa Kiingereza “English-Medium Schools”, hata kwa zile za elimu ya awali, tena nyingine ada ni lazima kulipwa kwa fedha za kigeni, hasa za Kimarekani, Dola! Kwa msingi huo, haitawezekana kuwa elimu hiyo “itahakikisha kudumishwa kwa maadili yetu ya kitamaduni”, kama yenyewe inatolewa kwa lugha ya kigeni ya kikoloni na kulipiwa kwa fedha za kigeni!.

Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, sehemu yake inasema: “Tanzania haina budi ijijengee misingi ya kujitegemea inayotokana na mazingira ya ukombozi wa kisakolojia, kifikra na kuweza kujiamini ili jamii iweze kuamua kuliongoza gurudumu lake la maendeleo kwa lengo la kutosheleza mahitaji ya msingi ya watu wote, wanaume, wanawake na watoto”. Je, tutaliweza hilo kwa kufundishia lugha ya kigeni, ya kikoloni?

Ni Siasa, Uchumi na Utamaduni

Karibu nchi zote duniani, zinatumia lugha zao kufundishia. Lakini katika Afrika karibu nchi zote (isipokuwa Ethiopia, inayotumia lugha yake ya Amharic na maandishi yake, pamoja na nchi za Kaskazini mwa Afrika zinazotumia Kiarabu na maandishi yake) zinatumia lugha za kigeni za Kiingereza, Kifaransa au Kireno, zilizorithiwa kutoka kwa Wakoloni hao. Haishangazi basi kuwa miaka 50 sasa tangu ukoloni uondoke, bado tunakuwa tegemezi kutoka kwa wakoloni hao.

Msomi B.F.P. Masele, katika makala yake yenye kichwa cha habari:

“Kiswahili au Kiingereza? Siasa na lugha muafaka ya kufundishiaTanzania,” alikariri “janga” lilioikuta nchi ya Afrika ya Madagaska iliyoamua mwaka 1975 kutumia lugha yake ya asili ya Kimalagasi, inayofahamika na kutumika kwa ufasaha zaidi nchini humo, katika nyanja zote za maisha ya watu, ikiwa ni pamoja na kufundishia elimu ya awali hadi vyuo vikuu.

Kwa mujibu wa Masele, baada ya Madagaska kukumbwa na hali mbaya ya kiuchumi, nchi ya Ufaransa, iliyokuwa ikiitawala zamani, ilishinikiza kuwa Kimalagasi kifutwe kama lugha ya kufundishia au kutumika katika shughuli nyingine rasmi kitaifa. Serikali, ikalazimika kukirudisha Kifaransa kuwa lugha kuu Madagaska baada ya kupewa ahadi ya fedha kutoka Ufaransa ili itatue matatizo yake ya kiuchumi. “Hili ni somo muhimu sana kwa Tanzania na nchi zote zinazofanana nayo”, anasema Masele.

Masele anaongeza: “Utekelezaji wa maamuzi ya matumizi ya Kiswahili kufundishia katika ngazi zote za elimu umekuwa mgumu ingawa jambo lenyewe liko wazi kiutafiti, kitaaluma, kipedagogia na kimantiki tangu zamani. Ugumu unatokana na ukweli kwamba, ingawa Kiswahili ni suala linalohusu lugha, mizizi yake ya fitina imejikita katika uwanja nyeti wa siasa, huku siasa hii ikifungamana na masuala ya uchumi na utamaduni. Bila ya kuichokonoa mizizi hii kutoka katika siasa, uchumi na utamaduni ilikojificha, si tu itakuwa vigumu, bali haitawezekana kukithamini Kiswahili”.

“Waafrika,” Masele katika makala hiyo amemnukuu mtaalamu mwingine nchini, M.M. Mulokozi akisema: “ni watu wa pekee duniani waishio kwa vitu vya kuazima; utamaduni wa kuazima, dini za kuazima, lugha za kuazima, majina ya kuazima, teknolojia ya kuazima, fasihi/fani za fasihi za kuazima, nywele na rangi za ngozi za kuazima, sanaa za kuazima, mavazi ya kuazima, vyakula vya kuazima…vitu ambavyo wengi wetu vinatufanya tuwe viumbe bandia, vichekesho vya dunia.”

Hivyo basi ni maoni yangu kuwa, kwa vile miaka 50 imekwishapita tangu uhuru bila ya kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia nchini katika ngazi zote, maandalizi yaanze sasa kwa kufundishia Kiswahili Sekondari na baadaye Chuo Kikuu. Kwa namna hii, utamaduni wetu utaendelezwa, vijana wetu wanaopata elimu watajijua vizuri wanatoka wapi na wanakwenda wapi na watakuwa na kitu cha kujitambulisha kama taifa. Isitoshe elimu itapanuka mno na taifa litapata wataalamu wanaoweza kujitegemea na wazalendo na hivyo utajengeka utamaduni wa kuwaamini wataalamu wetu na siyo wa nje. Ikifikia hapo, kasi ya maendeleo nchini itakuwa kubwa mno, kwa muda mfupi sana, kiajabu.

(mwisho)

• Saidi Nguba aliwahi kuwa Mhariri Mtendaji wa Magazeti

yanayochapishwa kwa Kiswahili ya UHURU (2000 – 2004) na Mwananchi

(2004 – 2005). Hivi sasa ni Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu. Haya ni maoni na mawazo yake binafsi.

Simu: 0754 -388418, Barua-Pepe: sanguba@gmail.com

7 comments:

Anonymous said...

George W. Bush inherited a strong economy, a budget surplus, and a nation at peace.

Eight years later, he left Obama with a shattered economy, a trillion dollar deficit, and two useless wars.

Obama saved the country from another Great Depression, rebuilt GM, reformed healthcare, reformed Wall Street, doubled the stock market, created 10 straight quarters of GDP growth, created 27 straight months of private sector job growth, got Bin Laden, got Gaddafi, and got us out of Iraq.

And now with the automatic spending cuts and the expiration of the Bush tax cuts in 2012, Obama has solved the deficit problem as well.

Obama has done a very good job.

joji said...

Hongera!

Ingawa mimi Mzungu nakuunga mkono.

Lugha yangu ni lugha ndogo. Wanaoelewa kiholanzi ni chini ya milioni thelathini. Lakini ni lugha ya kufundishia toka shule ya msingi mpaka chuo kikuu.

Kiingereza ni lugha ya kigeni. Muhimu, nakubali. Kinafundisha tangu shule ya sekondari. Kinatumika hasa wakati wa kuandika PhD. Bila kusahau kwamba Waingereza ni majirani yetu.

Tujivunie lugha yetu. Watanzania wajivunie Kiswahili,

joji said...

Ingawa mimi ni Mzungu nakuunga mkono.

Lugha yangu ni ndogo. Wanaoelewa kiholanzi ni chini ya milioni thelathini.

Lakini ni lugha ya kufundishia, tangu shule ya msingi mpaka chuo kikuu.

Kila kitu kwa kiholanzi : serikali, biashara, dini ...

Kiingereza ni lugha ya kigeni. Kinafundishwa tangu shule ya sekundari. Waingereza ni majirani wetu ...

Anonymous said...

Mimi ni Mtanzania, Watu watasema mpaka wachoke. Wanangu mimi nitajitahidi niwasomeshe shule zinazofundisha kiingereza.

Akili ni nywele kila mtu ana zake!

Kiswahili kinakunyima fursa za kujifunza. Kiswahili kinakuacha unapambana na wahindi mitaani humu na kunyanyaswa kwa ajira uchwara!

Anonymous said...

Kutumia lugha za watu wengine kuendeshea maisha yako ni kujitwisha mzigo usiobebeka. Kunajenga kutokujiamini katika kiwango cha juu kabisa. Ndiyo maana elimu ya darasani imeshindwa kabisa kumkomboa mtu mweusi. Utashi wa kisiasa unahitajika kuondoa hili tatizo.

Malkiory Matiya said...

Ni kasumba sawa lakini ni ukweli usiopingika kuwa Kiingereza itabakia kuwa lughu kuu ya kuunganisha binadamu wenye ndimi tofauti. Ndipo alipowazidi wanadamu wengine Mwingereza. Nadharia ni sawa lakini ukweli hutabadili.

Anonymous said...

1960's watoto wa Soweto walipigwa risasi wakiandamana kutaka elimu iwe sawa kwa waafrica na wazungu, ikumbukwe watoto wa kizungu walifundishwa kwa kiingereza wakati weusi walifundishwa kwa kizulu na lugha nyingine za kienyeji. Fikiria shule za academia wafundishe kiingereza na za kata kiswahili hivyo hivyo kwa vyuo vikuu.