Monday, April 09, 2012

Ratiba ya Mazishi ya Steven Kanumba

Steven Kanumba 1984-2012


RATIBA YA MAZIKO YA KANUMBA

Kamati ya mazishi ya msanii Steven Charles Kanumba jana jioni walitoa taarifa ya ratiba kwa vyombo vya habari ya utaratibu wa kumpeleka katika nyumba ya milele msanii huyo ambaye alikufa Ijumaa Aprili saba usiku.

Msanii huyo ambaye atazikwa katika makaburi ya Kinondoni amefanyiwa utaratibu ambao utamwezesha kila mwenye kuhitaji kushiriki mazishi hayo kuweza kumuaga. Mwili wa marehemu utachukuliwa kwa msafara kutoka hospitali ya Taifa Muhimbili saa 2.30 asubuhi. Utapitishwa barabara ya Umoja wa Mataifa na Ali Hassan Mwinyi hadi viwanja vya Leaders Club, Kinondoni ambako Misa ya kumuombea itasomwa pamoja na salamu mbalimbali kabla ya watu wote kumuaga. 

Kamati hiyo imetoa wito kwa watu kujitokeza kwa wingi kuanzia saa mbili asubuhi kumuaga katika barabara ambazo atapitishwa . Saa 3.30 asubuhi mwili wa Kanumba utapokelewa viwanja vya Leaders ukitanguliwa na mapokezi ya wazazi wake, viongozi mbalimbali wa serikali ambao juu yao kabisa atakuwa makamu wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dk Mohamed Gharib Bilal. 

 Saa 4.00 itakuwa ni muda wa kusoma Misa ambayo inakadiriwa kuchukua dakika 60 na saa 5 itakuwa kipindi cha salamu kutoka kwa watu mbalimbali. Saa 6.00 mchana ratriba ya kumuaga Kanumba itaanza mpaka saa 9.00 alasiri na baada ya hapo utakuwa wakati wa kuusafirisha mwili kwa msafara kutoka Leaders Club mpaka makaburi ya Kinondoni.Msafara huo utapitia barabara ya Tunisia, utakatisha barabara ya Kinondoni kuelekea makaburini. 

Sa 10.00 maziko yatafanyika kwa kufuata taratibu za imani ya marehemu. Kamati hiyo ya mazishi inayoongozwa na Gabriel Mtitu imewaomba wananchi watakohudhuria shughuli hiyo kwenda na maua ili kumuaga kwa heshima. Ibada na maziko vitafanyika kadri ya imani ya marehemu. Utulivu, unyenyekevu na ustahimilivu ni mambo muhimu yanayohitajika katika kipindi chote cha kumuaga mpendwa wetu Kanumba. 

BWANA ALITOA, BWANA AMETWAA. Sisi wote tulimpenda kwa dhati na tulitamani aendelee kuwa nasi siku zote ila Mungu aliyemleta kwa mapenzi yake ameamua kumchukua. Jina lake lihimidiwe. 

 K.N.Y GABRIEL MTITU MWENYEKITI WA KAMATI YA MAZISHI

..R.I.P STEVE KANUMBA

No comments: