Saturday, April 07, 2012

Rais Kikwete Atoa Salamu za Rambirambi - Kifo cha Kanumba


                    UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania –TAFF- kuomboleza kifo cha msanii maarufu nchini Steven Charles Kanumba, aliyeaga dunia usiku wa kuamkia leo, Jumamosi, Aprili 7, 2012.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete amemwomba kiongozi huyo wa TAFF kufikisha salamu za rambirambi za dhati ya moyo wake kwa wana-familia ya Kanumba na kwa wasaani wote nchini ambao wamepotelewa na mdau na mwenzi wao.
Rais Kikwete amesema kuwa ameshtushwa na kuzunishwa na kifo cha msanii huyo ambaye amemwelezea kuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye katika uhai wa maisha yake mafupi na akiwa bado kijana sana amechangia kwa kiwango kikubwa maendeleo ya sanaa ya filamu nchini na kupitia sanaa hiyo kuitangaza Tanzania kimataifa.
Amesema Rais: ”Nimepokea kwa mshtuko na huzuni nyingi taarifa za kifo cha Ndugu Steven Charles Kanumba. Kupitia filamu zake, ameburudisha na kuelimisha jamii yetu kwa namna ambayo haiwezi kupimika. Alikuwa msanii mahiri na mwenye kipaji kikubwa ambaye mchango wake mkubwa katika kuanzisha, kukuza na kuimarisha sanaa ya filamu nchini hautasahaulika.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Ndugu Kanumba pia ametoa mchango mkubwa katika kuitangaza nchi yetu ya Tanzania mbele ya mataifa mengine kupitia sanaa ya filamu na uwezo mkubwa wa kisanii. Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake huo kwa nchi yetu.”
Nakutumia wewe Rais wa TAFF salamu zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa wasanii wote wa filamu na sanaa nyingine kufuatia msiba huu mkubwa kwa fani yetu ya sanaa. Aidha, naomba unifikishie salamu za dhati ya moyo wangu kwa wanafamilia wote. Wajulishe kuwa niko nao katika msiba huu mkubwa. Waambie naelewa machungu yao katika kipindi hiki kigumu cha msiba,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
Namwomba Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu za kuweza kuhimili kipindi hiki kigumu kwa sababu yote mapenzi yake. Aidha, naungana na wana-familia na wasanii wote nchini kuwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke pema peponi roho ya Marehemu Steven Charles Kanumba. Amen.”
Mwisho.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
07 Aprili, 2012

2 comments:

HK said...

RIP Kanumba, umeondoka bado mtoto kabisa maskini, yaani kinyume kabisa na matakwa ya kibailojia. Binafsi kama mpenzi wa filamu na sanaa kwa ujumla, hususan ya kitanzania ninakufahamu personally na kimchango wako kwenye industry ya Bongo Movies, sina shaka na umahiri na uwezo wako wa hali ya juu. Pumzika kwa amani kaka! Tutaendelea kukuenzi kwa kujifunza kutoka kwako na kuendeleza mission yako

Nakumbuka kuna kipindi tulitaka kutengeneza filamu pamoja japokuwa haikufanikiwa kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wetu. Natamani tungefanikiwa ungekuwa umeniachia alama ya ukumbusho wako

HK,
Film Director, The African Shuga Mama, The One I Love, Penzi Kizungumkuti, Prof. Kazi na Dr. Mjusi (Commedy)

Anonymous said...

Tumempoteza mzalendo wa kweli. Ukiangalia mahojiano yake ambayo mzee Michuzi ali post siku chache zilizopita hata leo ame post tena inasikitisha. Kuna maneno mengi alitoa ya busara ambayo kusema kweli sisi watanzania inabidi tuyafuate. Watanzania wengi hatupendani, watu wana chukiana pasipo na sababu za msingi, tunakosa uzalendo, kuwa na roho mbaya kuto kufurahia maendleo ya mwenzako vyote hivi havi mpendezi mwenyezi mungu. Kwa kinywa chake yeye mwenyewe alituasa tupendane sisi watanzania na tuwapende na kuwapa vijana wetu au wasanii wetu na kuwapa support badala ya kuwakatisha tamaa. Mungu amsamehe yale yote aliyofanya kinyume na mapenzi ya mwenyezi mungu maana hapa duniani sisi binadamu ni dhaifu hamna ukamilifu, na ampokee kwenye pumziko la milele Amina.