Wednesday, April 11, 2012

Lulu Mahakamani Kisutu Leo!

Lulu Akijiandaa kuacti Sinema
Hayati Steve Kanumba ni miongoni mwa wasanii maarufu wa Tanzania wenye nyota za umaarufu (Tanzania Walk of Fame) ndani ya ukumbi wa Dar Live jijini Dar Es salaam ambapo mara baada ya kifo chake wafanyakazi wa ukumbi huo na mashabiki wake wameweka mashada ya maua,kadi na kuwasha mishumaa kama ishara ya kuomboleza kifo chake.
 (Picha kw Hisani ya Abdallah Mrisho Blog)
MAELEZO KUTOKA MICHUZI BLOG:

Muigizaji wa Filamu nchini anaehusishwa na kifo cha Muigizaji Mwenzie, Marehemu Steven Kanumba,Elizabeth Michael a.k.a Lulu amepandishwa kizimbani mapema leo asubuhi kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam kwa kusomewa mashtaka yake kuhusiana na kuhusika kwa kifo cha Muigizaji huyo nguli hapa nchini.


Elizabeth Michael amesomewa mashtaka hayo mbele ya hakimu Agustino Mmbando na wakili Elizabeth Kaganda ya mauaji ya Muigizaji wa Filamu nchini,Marehemu Steven Kanumba yaliyotokea huko sinza vatcan jijini Dar es Salaam april 7 mwaka huu.

Elizabeth Hakutakiwa kujibu chochote Mahakamani hapo kwani mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Kesi hiyo imeahirishwa na kupangwa kusikilizwa tena april 23 mwaka huu.

Muigizaji huyo aliletwa mahakamani hapo kwa mwendo wa kasi kama mshale na kwa ulinzi mkali na pia ndivyo alivyoondolewa Mahakamani hapo kiasi kwamba hakuna hata mwandishi alieweza kupata picha ya Muigizaji huyo mwenye tuhuma za mauaji Na kupandishwa katika gari ndogo nyeupe aina ya suzuki grand vitara yenye nambari za usajiri T 848 BNV huku kwenye kioo nambari zake zikisomeka PT 2565.

********************************************************************

Lulu kortini kwa kumuua Kanumba

Polisi wamficha, wakwepa waandishi
Ajifunika ushungi, avaa kandambili

Msanii wa uigizaji wa filamu nchini, Elizabeth Michael Kimemeta (18), maarufu kama Lulu, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka ya mauaji ya msanii mwenzake, Steven Kanumba (28).

Tukio la msanii huyo kufikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashtaka lilikuwa kama mchezo wa filamu baada ya polisi kufanya siri na hata kugombana na baadhi ya waandishi wa habari waliotaka kuingia katika chumba cha mahakama kufuatilia kesi hiyo.

Kesi hiyo ilisomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Augustina Mmbando.

Kabla ya kusomewa mashtaka hayo, hakimu alimtaka Lulu kutojibu chochote kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Wakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda, alidai kuwa Aprili 7, mwaka huu katika eneo la Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua Kanumba.

Kwa mujibu wa Mwenendo wa Sheria ya Makosa ya Jinai (CPA), Lulu hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.

Hata hivyo, mara upelelezi utakapokamilika, kesi hiyo itahamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusikilizwa.

Kaganda alidai upelelezi bado haujakamilika, hivyo akaiomba mahakama kupanga tarehe ya kuitajwa kwa kesi hiyo.

Hakimu Mmbando alisema mshtakiwa atakaa mahabusu hadi Aprili 23, mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa.

Wakati mshtakiwa huyo akisomewa hati ya mashtaka alidai mahakamani hapo kwamba, umri wake sio miaka (18) kama ilivyoandikwa kwenye hati ya mashtaka bali ana miaka (17).

Pia wakati mashtaka yanasomwa hali mahakamani hapo ilikuwa shwari, huku watu wengine wakinong’ona bila kuwa na uhakika kuhusu msanii huyo kufikishwa mahakamani kutokana na kutoonekana kwa wanafamilia wake na watu wa karibu.

Mazingira ya Lulu kufikishwa mahakamani hapo yalikuwa kama mchezo wa kuigiza kutokana na jeshi la polisi kufanya kuwa siri kubwa.

Gari aina ya Suzuki Vitara liliingia katika viunga vya mahakama hiyo muda ambao haukufahamika likiwa na makachero wa Jeshi la Polisi wanne, wanawake wawili na wanaume wawili na mshtakiwa.

Lilifuatiwa na gari lingine aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa na askari polisi saba waliovaa sare za jeshi hilo wakiwa na silaha.

Hata hivyo, baada ya muda NIPASHE kupitia chanzo chake ilipata taarifa ya msanii huyo kufikishwa katika viunga vya mahakama hiyo na kwamba jalada la kesi yake lilikuwa limeshapangiwa hakimu.

Hatua hiyo ilisababisha waandishi wa habari za mahakama kujipanga na kuweka lindo katika kila kona ya jengo la mahakama hiyo huku wengine wakiwa kwenye mlango wa kutokea mahabusu, kwenye korido za milango ya kuingia katika ofisi za mahakimu.

Hata hivyo, kundi la waandishi waliokaa katika korido ya ghorofa ya kwanza kuelekea kwenye ofisi za mahakimu, ghafla saa 5:20 asubuhi walifanikiwa kumuona mshtakiwa huyo akiwa katikati ya makachero wanawake wawili na nyuma wanaume wawili akiwa amejifunika ushungi wa rangi ya udhurungi, gauni kubwa maarufu kama ‘dira’ la rangi ya njano na kandambili za rangi nyekundu.

Waandishi hao walikimbilia msafara huo uliokuwa na askari wanne pamoja na mshtakiwa, lakini kabla ya kuingia chumba cha hakimu, askari aliyekuwa ameshika simu ya upepo mkononi aliwazuia waandishi kuingia.

Hali hiyo ilisababisha majibishano ya muda na mwishowe alibadili nia ya kuzuia wanahabari hao kufanya kazi yao.

Mshtakiwa alisomewa mashtaka yake na baadaye alipitishwa njia ya mlango wa nyuma hadi kwenye gari aina ya Suzuki Vitara yenye namba za usajili T848 BNV yenye vioo visivyoonyesha ndani (tinted).

Ingawa gari hilo lilikuwa na namba za kirais, kwenye vioo liliandikwa namba PT 2565, na iliondoka mahakamani hapo kwa kasi kumpeleka mshtakiwa mahabusu ya Segerea kusubiri upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Mapema jana saa 3:35 asubuhi, NIPASHE ilizungumza kwa njia ya simu na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Charles Kenyela kuhusu hatima ya kufikishwa mahakamani kwa msanii huyo, mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo:

NIPASHE: Shikamoo afande.

Kamanda Kenyela: Marahaba. Nipigie baadaye niko kwenye kikao.

NIPASHE: Sawa afande. Lakini nilitaka kujua kama Lulu atapelekwa mahakamani leo (jana) na itakuwa mahakama gani Kinondoni au Kisutu?

Kamanda Kenyela: Mmmh! Kwa kweli bado uchunguzi unaendelea. Hivyo, jalada liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).

NIPASHE: Ahsante afande. Shida yangu ilikuwa hiyo tu endelea na ujenzi wa Taifa.

Kamanda Kenyela: Nashukuru sana mwandishi.

Kanumba alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumamosi Aprili 7, mwaka huu, baada ya kudaiwa kutokea ugomvi kati yake na Lulu.

Maelfu ya watu, wakiwamo mawaziri, wabunge, viongozi wa siasa, vyama vya kiraia, wasanii wenzake na wananchi wa kawaida, walijitokeza katika msiba huo nyumbani kwake, Sinza Vatican, jijini Dar es Salaam na kwenye shughuli za kumuaga viwanja wa Leaders Club na kuuzika mwili wake katika makaburi ya Kinondoni.

Mazishi hayo yaliongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal.


CHANZO: NIPASHE

5 comments:

Anonymous said...

Kama Elizabeth Lulu Michael alitaka Umaarufu basi kaipata. Mpaka siku ya kufa kwake atajulikana kama binti aliyemwua Kanumba! Na sinema zake sitaki kuziona tena!

Anonymous said...

Lulu ameanza maisha mapya segerea leo mara baada ya kushuka kizimbani aliposomewa shtaka la mauaji ya SK...da maskn, no makeup, no mashauzi, no nyodo, no disco, no biere, no kanumba....akitoka marafiki zake watakuwa kakobe, mwingira, rwakatare, TB joshua......ataheshmu wakubwa mara elfu's

Kanumba Number 1 Fan said...

Nimeshindwa kutoa pole mapema kwa msiba wa Kanumba kwa sababu bado nilikuwa natafakari nini cha kusema. Kwa ukweli mimi ni mmojawapo wa wapenzi wa Kanumba katika filamu na kwa ukweli nilikuwa naangalia filamu zake na JB tu! wengine hawakuwahi kunishawishi labda pastor Muamba akikemea mapepo.
Kilichonisukuma kutoa pole leo ni tafakuri kwamba tutapoteza wasanii wangapi kwa uzembe?
Nilikuwa na classmate wangu NELLY. alianza mziki hip hop akaishia kufa kwa kuchomwa kisu. Leo nimempoteza Kanumba, Mr Nice kafulia hadi hatamaniki, Wema yeye ni vurugu usiku na mchana, Sinta alijiuza hadi akachokwa na sasa Lulu yuko lupango! Wasanii wetu wanaamini saa zingine kwenye umaarufu wa kuleteana mabifu! Nashindwa kuelewa kama bifu la Kanumba na Lulu lililopelekea msiba lilikuwa la kujenga umaarufu au ni lakweli!
Shida kubwa ni wasanii wetu kutokuandaliwa kuwa ma -SUPERSTARS. hatuwaandai kukabiliana na changamoto za jamii, hatuwaandai kwenye maisha bila kujulikana hadi kujulikana na wakati mwingine unakuwa maarufu sana lakini mfukoni huna kitu. Hatuwaandai kuwa mfano tunawaandaa kuwa kero. Leo Matunzo mabovu ya lulu yamemfikisha hapo alipo. Lakini kosa sio la lulu bali ni kosa la jamii! Lulu aanaamini kwamba kuwa mzuri ni kutembea uchi, Kanumba aliamini kuwa Star ni kutembea na wanawake wazuri wote! Jana WEMA leo Lulu kesho...?
Majanga kwa wasanii hayataisha tusipojipanga tutawapoteza wengi ama kwa kifo ama kwa magereza!

MYTAKE: Inatakiwa ijengwe shule (AMA BAGAMOYO INGEWEZA KUWA MAHALI SAHIHI) KWA AJILI YA WASANII WETU KUANDALIWA. HUKO WANGEJENGWA KISAIKOLOJIA NA PENGINE FAMILIA MASKINI WALIZOTOKA ZINGEWEZA KUFAIDI MATUNDA YA WATOTO WAO.

POLENI SANA KWA MSIBA WATANZANIA WOTE.

Anonymous said...

anony ,april 11,2012 11:21AM
UMENIFURAHISHA KWELI NA HUYU LULU AKITOKA SEGEREA KUOKOKA NDO SALAMA YAKE VINGINEVYO ATAISHI MAISHA MAGUMU SANA, bora aamue kuishi maisha ya kumcha Mungu tu.

Anonymous said...

Lulu went from seeking the Fame she so wanted to Infamy! All at the ripe old age of 17! Pole sana my dear.