Friday, February 08, 2008

Kumbe Lowassa hakupendwa! Nasikia watu walifanya parties za kusherekea kuondoka kwake. Tutajua huko mbele mambo yatakavyokuwa, lakini wazungu wanasema, "Be Careful What you Wish For".

Tuone kama pesa zilizopotea/kuibiwa zitapatikana na kurudishwa serikalini. Je, Serikali wata-sue hiyo kampuni ya Richmond Printerrs?*************************************************************************
Kutoka Ippmedia.com

Dar yazizima kwa furaha Lowassa kujiuzulu

2008-02-08

Na Waandishi Wetu

Jiji la Dar es Salaam, jana lilizizima kwa mayowe na vifijo vya furaha huku madereva hasa wa teksi, wakipiga honi baada ya kusikia Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake.

Miongoni mwa maeneo yaliyozizima kwa furaha ni ya benki ambako televisheni zilifunguliwa huku kipindi cha Bunge kikiwa kinaendelea wakati wa asubuhi. Maeneo mengine ni ya vituo vya mabasi ambako kuna migahawa iliyo na televisheni, watu walijazana kuangalia wabunge wanavyochangia sakata la Richmond huku hamu ya wengi ikiwa ni kusikia kauli zinazotolewa na wabunge baada ya Kamati Teule ya Bunge, kumtangaza Waziri Mkuu kuwa miongoni mwa watuhumiwa wakubwa wa mkataba bomu wa Richmond.

Wananchi wengi walijazana kwenye magari yenye redio kusikiliza kauli hiyo ya Waziri Mkuu. Katika Benki ya CRDB makao makuu, wafanyakazi wa benki hiyo pamoja na wateja waliokuwemo ndani kupata huduma, walilipuka kwa shangwe baada ya kumsikia Bw. Lowassa akitangaza azma yake ya kuachia ngazi.

Ilibidi hata huduma za benki hiyo zisimame kwa takriban dakika tatu kutokana na wafanyakazi wake kuziacha kompyuta na kuanza kuruka ruka wakionyesha hisia zao kutokana na uamuzi huo mzito wa Bw. Lowassa.

Kelele hizo ziliwashtua hata watu wengine ambao hawakuwa wakifuatilia mjadala huo wakidhani kuwa kuna jambo lisilo la kawaida limetokea. Hali kadhalika, wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), nao walisitisha masomo na kuanza kupiga kelele za furaha baada ya kusikia Bw. Lowassa ametangaza kumwandikia barua ya kujiuzulu Rais Jakaya Kikwete.

Vile vile, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaaam, walikuwa wamekusanyika makundi kwa makundi wakijadili kwa furaha, tangazo la Bw. Lowassa la kumwandikia barua ya kujiuzulu Rais Kikwete. Katika kujadili kwao, wanafunzi hao walitaka vigogo wengine waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo, kujiuzulu pia na sheria ichukue mkondo wake.

Katika eneo la Feri, nako hali ilikuwa hivyo hivyo kwani wachuuzi wa samaki walikusanyika huku wakishangilia kwa mbwembwe. Bw. Omar Abdallah aliishauri serikali kuwa, kujiuzulu kwa Waziri Mkuu isiwe ni danganya toto, kwani haitoshi, lazima sheria ichukue mkondo wake ikiwa ni pamoja na kutaifisha mali zake.

``Serikali iwawajibishe mawaziri wote waliohusika na ufisadi huu. Ameanza Lowassa anayefuatia awe Karamagi ili wananchi waendelee kuwa na imani na serikali yao,`` alisema Bw. Said Hussein. Naye

Bw. Athuman Bakari alisema kujiuzulu siyo sababu ya kukwepa kujibu tuhuma zinazomkabili. ``Aisee, unaweza kudhani ni Simba kamfunga Yanga au Yanga kamfunga Simba. Hii ni dalili kuwa wananchi wamechukizwa na ufisadi uliofanywa na kampuni hiyo ya Richmond kwani matokeo yake ni maumivu kwa wananchi kupandishiwa bei ya umeme.

``Tunashindwa hata kutumia vifaa vyetu kama majiko ya umeme kutokana na bei ya umeme kuwa kubwa,`` alisema Bw. Bakar Awadhi. Aidha kwenye daladala gumzo kubwa lilikuwa ni kauli ya Waziri Mkuu kuchukuwa uamuzi huo. Wengi walionekana kufurahia uamuzi huo, ingawa baadhi walimpongeza kwa maamuzi yake, ambayo ni nadra sana kufikiwa na viongozi wakubwa hasa wa Kiafrika.

SOURCE: Nipashe

No comments: