Tuesday, June 17, 2008

Wazee Waja Juu! - Kuugua kwa Dr. Harrison Mwakyembe


Huko kwetu kusini, kuna imani kubwa sana na mambo ya uchawi, si uongo. Wadau, sasa naona hii story ya Dr. Mwakyembe, itakuwa sinema kiboko hapo baadaye. Alivyowaumbua mafisadi na baada ya hapo kuugua ghafla na wazee wa kijijini kutokea kumsaidia.

***************************************************************

Kutoka ippmedia.com

Kuugua Dk. Mwakyembe: Wazee waja juu...!

2008-06-17

Siku chache tu baada ya Mbunge wa Jimbo la Kyela, Mhe. Dk. Harrison Mwakyembe kuugua ghafla wakati akiwa bungeni na kukimbiziwa kwenye zahanati ya ukumbi huo mjini Dodoma, limeibuka jopo la wazee mbalimbali maarufu mjini Kyela lililokuja juu na kudai kuwa kuumwa kwa mbunge wao huyo si bure na kwamba sasa wanajipanga katika kuhakikisha kuwa hadhuriwi na mambo ya kiuchawi.

Na kwa kuanzia, wazee hao wamesema tayari wameshaunda kamati ya wenzao kumi, ambao wamepiga kambi katika Kijiji cha Nduka kilichopo wilayani Kyela kwa ajili ya kupeana mbinu kali za kiulinzi kabla ya kufunga safari ya kuelekea Dodoma, ili hatimaye wakaonanane na mbunge wao huyo kipenzi na kumueleza kusudio lao la kumpa ulinzi kijadi.

Wakizungumza na PST mjini Kyela, wazee hao waliokataa kuandikwa majina yao gazetini kwa sababu walizodai kuwa ni za \'kiufundi\', wamesema kamati yao hiyo ya wazee kumi mahiri wa mambo ya kijadi, itaanza kwa kufuatilia kiundani ili kujihakikishia kile wanachoamini kuwa kweli, kuugua ghafla kwa mbunge wao huyo ndani ya Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumetokana na kulogwa.

``Baada ya hapo, kama itabainika kuwa ugonjwa uliompata (Dk. Mwakyembe) umetokana na mikono ya watu wanaokwazika na kazi yake ya kututetea sisi na Watanzania wengine, kitakachofuata ni kumganga na kisha kumtengenezea ulinzi imara ili asidhuriwe tena,`` akasema mmoja wa wazee hao.

Wakasema wamepata wasiwasi mkubwa juu ya kuugua ghafla kwa mbunge wao huyo, hasa baada ya kusikia habari za kuwepo kwa hofu ya vitendo vya kishirikina kufanyika ndani ya Jengo la Bunge.

``Tunajua kuwa siku zote Serikali haiamini mambo haya... na hata mheshimiwa si mfuasi wa mambo haya. Lakini yeye ni mtu wetu muhimu sana. Tukigundua kuwa alichezewa, sisi tutamlinda kwa namna tunayoijua hata kama mwenyewe akikataa,`` mzee mwingine akaongeza.

Alasiri ilipojaribu kuwasiliana na Dk. Mwakyembe ili kupata maoni yake kuhusiana na kikosi cha wazee hao kinachodai kutaka kumpa ulinzi maalum, hakuweza kupatikana kwenye simu yake ya mkononi. Hata hivyo, kuna taarifa kuwa sasa Dk. Mwakyembe yuko buheri wa afya na jana alirejea tena Bungeni kwa ajili ya kuungana na wenzie katika kuijadili bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha wa 2008/09.

Dk. Mwakyembe amejijengea heshima kubwa baada ya Kamati yake iliyotumwa na Bunge kufuatilia mkataba tata baina ya Serikali na Kampuni ya Kuzalisha Umeme ya Richmond kuibua udhaifu mwingi, ambao mwishowe ulimfanya Waziri Mkuu Edward Lowassa na mawaziri wengine watatu kujiuzulu.

Aidha, umahiri wake ulimfanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bwana Jakaya Kikwete amteue kuwa mmoja wa wajumbe waliounda Tume ya Jaji Bomani iliyopitia mikataba ya Madini na kuwasilisha mapendekezo yake (kwa Rais) hivi karibuni.

SOURCE: Alasiri

No comments: