Friday, June 13, 2008

Ugua Pole - Dr. Harrison Mwakyembe

Dr. Harrison Mwakyembe

Wadau huko wenye habari za kuugua kwa Dr. Harison Mwakyembe atupe. Dr. Mwakyembe na ripoti yake kiboko juu ya ufisadi wa Richmond ndo iifungua mlango wa kupiga vita ufisadi Tanzania.

Tunamwombea apone haraka.

******************************************************************************
Kutoka ippmedia.com

Dk. Mwakyembe: Hali yake bado tata

2008-06-13

Na Mwandishi Wetu,Dodoma

Hali ya afya ya Mbunge wa Jimbo la Kyela mkoani Mbeya, Mhe. Dokta Harrison Mwakyembe bado haijaimarika na watu wake wa karibu wamesema bado anaendelea na matibabu.

Mbunge huyo aliyeibuka kuwa shujaa hivi karibuni baada ya kuiongoza kwa umahiri Kamati ya Bunge iliyoanika siri zote kuhusu dili za mkataba wa utata baina ya Serikali na Kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond, ameelezewa kuwa hali yake haijatengemaa tangu jana aliposhikwa na ugonjwa ghafla akiwa bungeni na kulazimika kutoka nje ya ukumbi.

Imeelezwa zaidi kuwa hadi sasa, kile kilichomfanya Dokta Mwakyembe azidiwe ghafla na kulazimika kutoka nje ya Bunge jana hakijafahamika. ``Bado hajawa ok kwa asilimia mia moja... ila anendelea vizuri,`` amesema mmoja wa watu walio karibu na Mbunge huyo.

Alasiri ilipojaribu kuzungumza na baadhi ya wabunge wenzie, imebaini kuwa Mheshimiwa Dokta Mwakyembe ameanza kupata nafuu kulinganisha na hali aliyokuwa nayo jana baada ya kulazimika kutoka kwenye ukumbi wa Bunge.

Akizungumza na Alasiri leo asubuhi, Mbunge wa Mbeya Mjini (CCM), Mhe. Benson Mpesya, amesema ni kweli Mbunge mwenzie huyo aliumwa ghafla jana wakati akiwa Bungeni, lakini hivi sasa hali yake inaendelea vizuri. ``Ni kweli Dkt. Mwakyembe aliugua ghafla... lakini ni kazi ngumu kuzungumzia afya ya mtu. Ila ukweli wa yote ni kwamba jana usiku, mimi nilikwenda nyumbani kwake kumjulia hali na akanithibitishia kuwa hivi sasa amepata nafuu kubwa,`` akasema Mhe. Mpesya.

Aidha, Mhe. Mpesya amesema wananchi wa Jimbo la Kyela na kwingineko nchini wasiwe na hofu na afya ya Mhe. Mwakyembe, kwani kwa kauli yake (Dk. Mwakyembe), ni kwamba hali hiyo ya kuumwa ghafla Bungeni jana ilitokana na ukweli kuwa hakuwahi kupata kifungua kinywa jana wakati akienda bungeni.

``Hali hiyo ilimssababaishia kizunguzungu na ndiyo maana akaumwa ghafla,`` akasema Mhe. Mpesya. Naye Mbunge wa Lupa (CCM), Mhe. Victor Mwambalaswa, ambaye lidaiwa kuwa ndiye aliyekuwa wa kwanza kubaini hali hiyo na kumuondoa ndani ya Bunge Dk. Mwakyembe huku akimshikilia, amesema si kweli kwamba alihusika kumtoa nje ya Bunge.

``Ndugu yangu, hata mimi nasikia tu kuwa Dk. Mwakyembe anaumwa... ukweli ni kwamba sijui hata alikolazwa na wala sijui anaugua nini,`` amesema Mhe. Mwambalaswa. Jitihada za mwandishi wa Alasiri kumpata Dk. Mwakyembe mwenyewe zilishindikana kwa jana na leo, hasa baada ya simu yake ya mkononi kutoweza kupatikana.

Dk. Mwakyembe ambaye umahiri wake umemfanya hivi karibuni awe miongoni mwa wajumbe walioandaa ripoti kuhusu mikataba ya madini nchini baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bwana Jakaya Kikwete, ameripotiwa kuwa jana mishale ya saa 3:30 asubuhi, aliumwa ghafla wakati akiwa ndani ya ukumbi wa Bunge na kukimbiziwa kwenye zahanati yao Bungeni hapo.

SOURCE: Alasiri

3 comments:

Subi Nukta said...

Da Chemi, maelezo mengine yapo kwa kaka Msimbe wa Lukwangule Ent. hapa: http://lukwangule.blogspot.com/2008/06/dk-mwakyembe-yu-fiti.html

Subi Nukta said...

Haya tena Da Chemi,
Habari za kuugua Mwakyembe hizi hapa kutoka gazeti la Majira.
Sijui aliyetulaani na habari za kusingiziana na kufanyiziana vitimbi WaTanzania ni nani maana inakuwa kama tupo mashindanoni vile. Ah!


Mbunge 'amwekea' uchawi Mwakyembe

*Kamera bungeni zamnasa 'akimwangia' kitini
*Spika, Naibu na wajumbe wa kamati nao wamo
*Mwakyembe azushiwa kifo, arejea Dar kuchunguzwa

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SIKU moja baada ya Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe, kuugua ghafla bungeni sasa imethibitika kwamba suala hilo lina uhusiano wa moja kwa moja na watuhumiwa wa ufisadi na tayari vyombo vya usalama vimeanza kulifanyia kazi.

Kuhusishwa moja kwa moja kwa watuhumiwa hao wa ufisadi na kuugua kwa Dkt. Mwakyembe, unatokana na mmoja wao kunaswa na kamera za chombo kimoja cha habari (jina tunalo) zilizoko bungeni.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alinaswa na kamera hizo akifuatana na Ofisa wa Bunge na kuweka vitu vinavyoaminika kuwa ni dawa za kienyeji katika kiti cha Mbunge huyo cha Spika wa Bunge Bw. Samwel Sitta, Naibu wake Bibi Anne Makinda, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Kuchunguza tuhuma za Richmond Bibi Stela Manyanya, Mbunge wa Same Bibi Anne Kilango na wabunge wengine.

“Unajua hatukuamini macho yetu, tulishangaa sana kumwona Mheshimiwa huyo akiwa na mmoja wa maofisa wa Bunge wakiingia na kuweka vitu fulani kwenye kiti cha Dkt. Mwakyembe, Spika, Stela Manyanya, Naibu Spika, Anne Kilango-Malecela na baadaye kwenye viti vya baadhi ya wabunge.

“Wakati huo kamera ya chombo husika ilikuwa 'on' kwa majaribio, kamera za Bunge zilikuwa zimezimwa, kwa kuwa muda ulikuwa bado kidogo, hawa ni wajanja sana, waliingia muda mfupi tu baada ya watu wa usalama kumaliza kukagua ukumbi," kilisema chanzo chetu ndani ya Ofisi ya Bunge.

Kilisema kitendo hicho kilimpa hofu kubwa pamoja na mwenzake waliyekuwa naye, hivyo kuamua kutoa taarifa hiyo kwa Spika.

Akizungumza na Majira jana, Bw. Sitta alikiri kutokea kwa tukio hilo na kueleza kwamba amesikitishwa na kitendo hicho, ambacho hakutarajia katika maisha yake kama kinaweza kufanywa na mtu mwenye akili na kiongozi aliyechaguliwa na wananchi.

“Kwa kweli taarifa hizo zipo na zimezagaa hapa mjini, mimi mwenyewe nimesikitishwa sana na tayari vyombo vya usalama vimeanza kufanya uchunguzi juu ya suala hili. Hatuwezi kuacha hivihivi katika mazingira kama haya...ni matukio ya kijingajinga tu hivi, ila hatuwezi kuyaacha hivihivi,” alisema Bw. Sitta.

Alisema hatua zitakapochukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao itajulikana baada ya uchunguzi wa kiusalama kukamilika na kwamba tayari Ofisa wa Bunge ameshahojiwa juu ya tukio hilo.

Kwa kawaida maofisa wa usalama hupita mapema ndani ya ukumbi wa Bunge kukagua kila eneo wakiwa na vitendea kazi kadhaa za kubaini kitu chochote kabla ya saa 2 asubuhi.

Dkt. Mwakyembe alirejea mjini Dar es Salaam jana kwa kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa afya yake. Hata hivyo jana ulizushwa uvumi kuwa Mbunge huyo amepoteza maisha, ambapo chumba cha habari cha gazeti hili kilipokea simu kadhaa zikiulizia hali hiyo.

Anonymous said...

Tunajua siku nyingi kuwa Bongo uchawi hadi Bungeni. Lakini hii aibu. Na huyo aliyemwekea dawa afukuzwe Bungunei mara moja!