Monday, August 11, 2008

Mwizi auawa Dar!

Mara ngapi umewahi kushuhudia mwizi anapigwa na wakati mwingine anapigwa hadi kufa. Wakati mwingine si mwizi ila basi tu mtu alikuwa ana visa na mtu anasema, "mwizi huyo!" basi jamaa anapata kipigo.

Niliwahi kuona mwizi anapigwa hadi kufa Ubungo miaka ya 90. Polisi walivyofika, moja alisema kwa utani, "asante kwa kutupunguzia kazi!" Loh!

****************************************
Kutoka ippmedia.com

Mtuhumiwa wa wizi Dar auawa

2008-08-11

Na Usu-Emma Sindila, Jijini

Mtu mmoja anayesadikika kuwa ni kibaka ameuawa kinyama na wananchi wenye hasira huko Mbagala baada ya kuchomolewa toka katika chumba cha wauguzi alikokuwa amejifika katika zahanati ya wazazi ili kujiokoa.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, Emmanuela Kandihabi, ameiambia Alasiri mapema leo asubuhi kuwa, tuki hilo limetokea jana mishale ya saa 4:00 usiku pale Mbagala Kizuiani katika Zahanati ya Wazazi.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Kandihabi amesema, kwa mujibu wa mtoa taarifa ambaye pia ni Muuguzi katika zahanati hiyo, Merina Kuitika, amedai kuwa akiwa kazini alishtukia mtu akiingia ghafla hospitalini hapo na kuingia katika chumba cha kubadilishia nguo manesi na kisha kujifungia.

Amesema akiwa bado hajang'amua nini kinachoendelea, alishtukia umati mkubwa wa watu ukijitoma ndani ya zahanati hiyo huku wakipiga kelele za mwizi, na kisha kwenda kuuvunja mlango wa chumba hicho na kumchomoa mtu huyo.

Kamanda Kandihabi amesema baaada ya kumchomoa mtu huyo walianza kumpiga kwa mawe na fimbo hadi alipofariki dunia. Amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Temeke.

SOURCE: Alasiri

No comments: