Wednesday, October 22, 2008

Ya Kale Dhahabu


Wadau, nilopokuwa nasoma Zanaki Girls 1977, amri ilitoka ya kuchoma vitabu vyote vilvyoachwa na Aga Khan Girls. Zanaki ilikuwa Aga Khan Girls kabla ya kutaifishwa. Vitabu vilikuwa vingi. Kulikuwa na vitabu vya hesabu, literature, Shakespeare, English na masomo mengi. Nilikuwa Form One na walikuwa wanavichoma kwa vile vilikuwa na kasumba! Tuliletewa vitabu vya Tanzania curriculum, hivyo literature badala ya Shakespeare na wengine tulisoma African writer's series. Ten a wakati tunachoma hivyo vitabu, kupata hata za kiswahili ilikuwa shida kidogo. Hizo zilizochomwa zingetusaidia anagalau.

Mnakumbuka enzi zile, eti ukiongea kiingereza unatukanwa eti una kasumba! Ilikuwa enzi za kukuza Kiswahili kuwa lugha ya taifa. Matokeo yake watu waliokuwa wanajua kiingereza walifanya kuwa hawajui! Matokeo yake wabongo wengi wanaongea kiingereza kibovu kwa vile walifundishwa na walimu wasioelewa lugha vizuri.

Dada Subi ameniletea habari za kusikitisha. Ni tukio uliotokea alipoenda kwao. Alikuta vitabu vya kiswahili vimechomwa! Khaa! Jamani, kwa nini vitabu vichomwe??? Si zina gharama. Yaani hazina faida tena? Hata hapa Marekani hawachomi vitabu vinapelekwa second hand store au zinasafirishwa nchi za nje.

*******************************************************************

Imeandikwa na Dada Subi:

Ya kale dhahabu!

Mimi nilipokuwa Tanzania majuzi niliwenda hadi shule yangu ya Msingi kumwomba Mwalimu Mkuu vitabu vya zamani, hadithi niliyopewa nilichoka. Ati Waalimu wakuu wa shule za msingi wote walipewa amri toka kwa Waziri wavichome vitabu vya zamani ili kutoa nafasi kwa vitabu vipya. Huyo waziri mbumbumbu sijui alitamka akiwa amelewa buza ama gongo gani. Kumbuka zile stoo za vitabu zilivyokuwa zimejaa vitabu, vyote vikapigwa kiberiti. Najiuliza, kwa nini hakuwepo mjanja mmoja akahifadhi nakala moja moja?

Nina imani atakuwepo mtu mmoja mmoja aliyeficha kimoja na mwingine kingine na siku moja tutaviona tena na vitauzwa kwa bei nzuri kweli. Nilipambana na maboksi ya vitabu vya Bibi na Mama kwa kuwa wao walikuwa Waalimu, wakanifahamisha kuwa sitafanikiwa kuvipata kwani wao walikuwa watiifu, hawakuchukua mali ya Shule/Serikali na kuihifadhi kama yao.

Kila mara huwa nakumbuka:
Juma na Roza. Someni kwa Furaha, hatua ya tatu.
Hadithi za Pazi na Jogoo alivyomning'iniza kichwa chini miguu juu, na ile hadithi ya Mwanamke aliyevalia hereni kubwa kisha akaenda sokoni kuuza bidhaa zake mara mbuzi wakapita wakarusha mguu ndani ya tundu la hereni nayo ikalikata sikio....
Unamkumbuka Kalumekenge alipokataa kwenda shule? Fimbo ikaambiwa imchape Kalumekenge ili Kalumekenge aende shule. Lakini fimbo ikakataa kumchapa Kalumekenge aliyekataa kwenda shule. Moto ukaambiwa uichome fimbo ili fimbo imchape Kalumekenge ili Kalumekenge aende shule. Lakini moto ukakataa kuichoma fimbo, iliyokataa kumchapa Kalumekenge, aliyekataa kwenda shule. Ndipo maji yakaambiwa yauzime moto, uliokataa kuichoma fimbo, iliyokataa kumchapa Kalumekenge, aliyekataa kwenda shule. Ndipo maji yaka kuuzima moto, moto ukaichoma fimbo, fimbo ikammchapa Kalumekenge, ndipo Kalumekenge akaenda shule.

Unawakumbuka Wagagagigikoko?

Unamkumbuka yule mtoto aliyetumwa kwenda kwa Bibi yake akacheza barabarani hadi simba akamla Bibi yake na kulala kitandani halafu yule mtoto alipofika akamwuliza, Bibi mbona masikio yako makubwa? Bibi akamjibu, ili niweze kukusikia vizuri. Akamwuliza tena, mbona macho yako makubwa? Akamjibu, ili niweze kukuona vizuri. Akamwuliza, mbona meno yako makubwa? Akamjibu, ili niweze kukutafuta vizuri. Ndipo akaiona miguu yake na simba akamrukia na kumla.....

Nikakumbuka na hadithi ya Usiku wa Mbalamwezi, na kabla ya hiyo ilikuwepo hadithi ya Muro na mifugo yake, halafu ilikuweko 'Leo ni Sikukuu' wachilia mbali ile hadithi ya mjukuu aliyekuwa anataka kushindana na babu yake kunywa chai lakini kumbe chai ni ya moto, basi babu yake akawa anatoa sababu ambazo zilikuwa zinaishia na neno 'fu' na kila aliposema 'fu' alipuliza chai 'fu fu fu'....

Mi nilikuwa nasoma na kurudia zile hadithi hadi nyumbani. Bibi kwa vile alikuwa Mwalimu, basi alikuwa akiazima kitabu kwa niaba yang nami nakisoma nyumbani na kukikabishgi ili kirudishwe kabla Ijumaa makusudi nisikose kuazimwa wiki inayofuata. Nilikuwa nasoma hadi mwisho na nyuma ya kitabu, jalada, kabisa nahakikisha nimesoma kujua kama kitabu kile kina chapa ya MTUU, TPS, Oxford, Longman ama Maximillian Publishing!

Unakumbuka hesabu zilivyokuwa zimepangika kwenye vitabu halafu pembeni zina picha zinazoendana na hisabu yenyewe?

Halafu somo la mwandiko nimemkumbuka mwalimu alikuwa anatufundisha kuumba herufi kwa wimbo, 'chirioooo cha, chirioooo cha....'

Eh jamani! Wametupa jongoo na mti wake! La haula la kwata!

Nasikitika sana mimi lakini najipa moyo kuwa ipo siku tutaviona tena vitabu vyenye hadithi na mafunzo murua...

Golden Days Are Gone? Aaaarrrrrrrgh!
Memories are made of this!

Subi

2 comments:

Anonymous said...

Subi umetukumbusha mbali sana!! Simile na motokari yangu? Paulo usije kucheza na sisi una mikono michafu? Makari hodari kaenda safari kampiga kimamba?
Kama ulikuta wanachoma vitabu kama hivi basi sisi kweli tuna matatizo!

Anonymous said...

Asante sana dada subi na chemi mmenikumbusha mbali sana enzi za bulicheka na wagagagigi koko. natumai unamkumbuka bwana matata pia