Friday, August 15, 2008

Chacha Wangwe aibuka toka Kuzimu

Wadau, niliona hii huko World Press. Kwa kweli maneno ni mazito si mchezo:

*********************************************************************
Kutoka
http://tarishi.wordpress.com/2008/08/

Chacha Wangwe aibuka toka kuzimu

Filed under: habari ndio hiyo — tarishi @ 12:15 pm

JARIDA LA CHACHA ZAKAYO WANGWE MBUNGE WA TARIME CHADEMA

Utangulizi:

Jarida hili la Mheshimiwa Chacha Zakayo Wangwe lina sehemu tatu. Sehemu ya kwanza litaweka bayana na kufafanua sababu za mimi kuchafuliwa kisiasa na baadhai ya viongozi wa ngazi za juu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, na sehemu ya pili itaonyesha baadhi ya maswali ya msingi niliyopata kuuliza Bungeni na majibu yake na sehemu ya tatu itakuwa na michango mbalimbali niliyopata kuchangia kwa muda wa miezi miaka miwili na nusu.

Lengo hasa la Jarida hili ni kumwelewesha Mtanzania na hususan MWANADEMOKRASIA juu ya tuhuma zilizoelekezwa kwangu kwa lengo la kunichafua kisiasa huku viongozi wa CHADEMA wakidai kukisafisha chama jambo ambalo si kweli na ni kampeni chafu zilizoandaliwa na baadhi ya viongozi wa Chama na kuwarubuni wajumbe 31 wasiokuwa wanademokrasia na kunipaka matope ya siasa zao zisizo na hata chembe ya Demokrasia.

Nasema hivi nikijua wazi kwamba, CHADEMA kama chama kinaendeshwa kwa katiba na kwa wakati huo huo kikiwa kinaendeshwa kidikteta na kauli za NDIYO MZEE. Ninajua wazi kwamba, viongozi wa sasa wa chama changu wanatofautiana sana na viongozi wa mwanzo wakati CHADEMA ikianzishwa kwani wanatofautiana kiitikadi, kisera na hata kimtazamo. Kwa mfano, mzee Mtei alikuwa akikieneza chama hasa vijijini miaka ya 95 kwa kutumia magari chakavu na alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwashawishi wananchi na wakijua kuwa CHADEMA si chama cha mjini, na hapa ndipo mwanzo wa CHADEMA kuwa Chama Tawala kule Tarime hadi sasa. Ila katika uongozi huu wa kizazi kipya basi kila kitu kinaenda kwa kauli za “Mheshimiwa Mwenyekiti kasema” na matumizi mabaya huku ufisadi ukikitafuna chama kwa matumizi hewa na kwa kigezo kuwa eti wanajilipa madeni ya Kampeni. Nililia sana juu ya matumizi ya helkopta katika kampeni lakini nikaanza kuonekana kuwa mini ni mbaya. Binafsi sikuona sababu za Chama kutumia helkopta ilhali bado wanachama wa vijijini hawakijui chama wala sera zake huku viongozi wa wilaya na mikoa wakishindwa hata kutoa durufu (photocopy) za viepeperushi vya chama kwa kukosa ruzuku. Hii si sawa.

SEHEMU YA KWANZA

Sababu za baadhi ya Viongozi wa CHADEMA kuamua kunichafua kisiasa.

Baadhi ya Kampeni za chini chini dhidi yangu, tarehe 28 na 29 Juni 2008 katika kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Dodoma ambacho kiluhudhuriwa na wajumbe 31 kiliridhia mimi kuondolewa kwenye wadhifa niliokuwa nao ndani ya chama kama Makamu Mwenyekiti kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutuhumiwa kuwa navujisha siri za chama kwa CCM. Binafsi kwangu kama mwanasiasa wa kiwango cha juu ni pigo kubwa sana kisiasa kuchafuliwa na watu 31 tu ndani ya chama. Ninachokiamini hapa ni kwamba, kutokana na msimamo wangu wa siku nyingi hata kabla sijawa makamu mwenyekiti CHADEMA, ndiyo sababu rasmi ya kupigiwa kampeni na baadaye kura za kutokuwa na imani na mimi kwa taarifa nilizo nazo ni kwamba anaandaliwa Dr. Slaa kushika nafasi hiyo. Hapa ikumbukwe kuwa Mke wa Dr. Slaa ni diwani kupitia CCM hivyo kuna uwezekano wa sera za chama zikavuja kupitia Mama huyu katika njia mbalimbali.

Ofisi ya Katibu Mkuu (Ofisi ya Slaa) ndiyo ya kwanza kunituhumu kuwa nawaingilia majukumu yao katika suala zima la matumizi mabovu ya fedha za ruzuku ya chama. Chama hupata zaidi ya milioni 60 kila mwezi. Ni fedha nyingi sana kukijenga chama kama zikipata mipango mizuri na kuachana na matumizi mabovu kama matumizi ya helkopta kwenye kampeni kama ilivyotokea kwenye chaguzi zetu pamoja na baadhiya viongozi kudai kuwa wanajilipa madeni waliokikopesha chama wakati wa kampeni za 2005.

Mhe. Philemon Ndesamburo Mbunge wa Moshi Mjini inadaiwa kuwa anakidai chama milioni 100 alizokopesha wakati wa kampeni za 2005.

Mhe. Philemon Ndesamburo Mbunge wa Moshi Mjini inadaiwa kuwa anakidai chama milioni 100 alizokopesha wakati wa kampeni za 2005, Freeman Mboe ambaye hadi sasa ni Mwenyekiti wa chama changu katika ngazi ya Taifa naye kwa taarifa nilizo nazo ni kwamba kila mwezi hulipwa shilingi milioni 10 ili kufidia fedha anazodai kukikopesha chama ambazo ni zaidi ya milioni 500 katika kampeni hizo hizo na hadi sasa anaendelea kukidai chama mamilioni ya shilingi.

Mimi nilipoonyesha wasiwasi juu ya madeni haya yasiyoisha, ikaundwa tume ya kampeni za kutokuwa na imani na mimi. Binafsi sijui kama viongozi wanaojiita makini kama kina Dr. Slaa na Kabwe Zitto wangeweza kuusimamia ufisadi mkubwa kama huu ndani ya chama huku wakiwa mstari wa mbele kuwafichua mafisadi Serikalini. Au ni kawaida kuwa Mganga hajigangi? CHADEMA kuna ufisadi wa aina nyingi sana kuanzia uchapaji bendera hadi manunuzi ya vifaa vya chama!

Katika ofisi ya Vijana nako kunanuka ufisadi kwani ni vijana wachache sana ambao hupata nafasi ya kwenda nje ilhali mikoani nako kuna vijana wanaohitaji kujifunza. Ofisi hii ina watu maalumu wa kwenda kwenye Semina na Matamasha mbalimbali. Na watu hao hupangwa na John Mnyika.

Pamoja na hayo, Kurugenzi hii inayoendeshwa na John Mnyika imekuwa ikifanya hesabu za “Mbili mara Mbili toa nne”. Nakumbuka matamasha mbalimbali yaliyowahi kuratibiwa na Kurugenzi hii kwa kutumia fedha za chama yamekuwa hayana maslahi yoyote kwa chama ….labda kwake mwenyewe kwani itakumbukwa kwamba Kurugenzi ilizindua mfuko ulioitwa Tumaini jipya Septemba 16, 2007 katika hafla ya wafanyakazi vijana na akaunti ya Tumaini Jipya 01810301 NBC ilifunguliwa. Jumla ya shilingi milioni 6,176,500 zimekusanywa na shilingi milioni 6,064,300 zimetumika kwa shughuli mbalimbali za vijana ikiwemo gharama za hafla yenyewe. Hafla nyingine kama hiyo ilifanyika Arusha.

Hafla hii ilifanyika tarehe 29 Machi, 2008 The New Polygon Triangel Arusha na kuhudhuriwa na washiriki 67 mgeni rasmi akiwa Mhe. Mzee Edwin Mtei. Jumla ya shilingi milioni 2,300,700 zilikusanywa na shilingi milioni 1,885,000. Zimetumika kwa shughuli mbalimbali za vijana ikiwemo gharama za hafla yenyewe. Sasa najiuliza, kulikua na mantiki gani ya kutumia fedha za chama kiasi cha shilingi 6,064,300 na kukusanya shilingi 6,176,500/=? Ni faida ya shilingi ngapi ilipatikana kama ameamua kukiingiza chama katika kufanya biashara ya matamasha?

Jingine, tangu nimekuwa mbunge Chadema na Baadaye Makamu Mwenyekiti sijawahi kuandaliwa safari za kibunge ama za kukiwakilisha chama ilhali kuna watu wasio na uwezo kiakili, kifikra na hata nafasi za uongozi lakini waliandaliwa safari za nje. Chama kimefikia hatua ya kuwakilishwa kimataifa na watu wasio na vigezo kwa ajili ya utawala mbovu! Siandiki haya kwa kuwa nimeondolewa katika uongozi, hapana! Hizi ni harakati zangu za muda mrefu juu ya utawala bora. Tazama, wafuatao wamewahi kusafiri katika mataifa mbalimbali kwa shughuli mbalimbali kukiwakilisha chama. Mhe. Suzan Lymo (Mb. Viti maalumu) Cape Towan, Afrika Kusini kwa Mkutano wa Interparliamentary Union. Susan pia amesafiri kwenda USA kwa High Level meeting ya HIV/AIDs mwezi June, 2008. Mhe. Zitto Kabwe, (Mb) alisafiri kwenda Berlin mara mbili – Mhe. Zitto pia alisafiri kwenda Marekeani kwa wiki 3 kwa mwaliko wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani pamoja na Wabunge vijana toka dunia nzima ambako walipata nafasi ya kutembelea majimbo mbalimbali ya Marekani. Mhe. Mhonga Said (Mb – Viti maalum) alisafiri kwenda Burundi kwa Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu. Mhe. Dr. Slaa amesafiri kwenda Johannesburg, Windhoek na Manzini Swaziland kwa vikao vya Kamati na Bunge la SADC. Dr. Slaa ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya InterParliamentary Cooperation Committee ya Bunge la SADC. Mhe. Maulida Komu (Mb. Viti Maalumu) alisafiri kwenda Nairobi na pia Finland. Mhe. Ndesamburo (Mb) alisafiri kwenda Australia kama Commissioner wa Bunge.

Wafuatao walisafiri kichama; Mhe. Mhonga Said (Mb – Viti Maalum), Maulida Komu (Mb – Viti Maalum), Suzan Kiwanga (Afisa Msaifizi Idara ya Uchaguzi na Kampeni) na John Mnyika Mkurugenzi wa Idara ya Vijana) walisafiri kwenda Norway na Sweden. Anthony Komu (Mkurugenzi wa Fedha na Utawala) alisafiri kwenda Norway kwa mwaliko wa Centre Party, Mhe. Balozi Ngaiza (Mjumbe wa heshma wa kamati kuu wa kuteuliwa na Mwenyekiti), John Mnyika (Mkurugenzi katika Ofisi ya Vijana), John Mrema (Afisa katika Kurugenzi ya Halmashauri na Bunge), walisafiri kwenda Windhoek Namibia kwa Mkutano wa Dua, na Mhe. Kimesera (Katibu Mtendaji wa kuteuliwa na Mwenyekiti), Suzan Lymo (Mb) Viti maalum, na John Mrema walisafiri kwenda Kampala, Uganda kwa Mkutano wa Dua.

Ndugu Regia Mtema (Afisa katika Kurugenzi ya Vijana) alisafiri kwenda Malawi kwa Mkutano wa NIMD. Mama Naomi Kaihula (Mkurugenzi katika Idara ya Wanawake) na Regia Mtema walisafiri kwenda Finland kwa mwaliko wa Shirika la Demo Finland. Johna Mrema, Msafiri Mtemelwa na Happiness Mwaipopo (Sina hakika kama ni Mwanachama) walisafiri kwenda London/Uingereza kwa mwaliko wa Conservative Party/WFD wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mhe. Benson Kigaila (Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo) alienda Zimbabwe katika uchaguzi uliofanyika 27 June, 2008 kupita Ofisi ya Msajili wa Vyama.

Suala la ukabila ni jambo ambalo halihitaji kupingwa kwani asilimia karibu 85 ya viongozi wa CHADEMA wametoka katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha pamoja na kwamba baada ya mimi kulishupalia jambo hili wameanza kubadilisha majina.

Wapo wanachama kama mimi ambao nao wakipewa nafasi za uongozi ndani ya chama hiki watafanya vizuri zaidi ya hawa na wengine ambao ni Jobless! Pengine niweke wazi hapa kuwa, mimi ni kiongozi shupavu nisiye kuwa na hata chembe ya woga katika kuteta na kusimamia haki za mwanachama wa CHADEMA tena nisiyependa siasa za kisanii. Ukweli huu ndio uliowafanya kina Mbowe, Slaa kuwa mstari wa mbele katika kupiga kampeni na baadaye kura ya kutokuwa na Imani na mimi. Binafsi naamini katika chama cha siasa mtu muhimu ni Mwanachama na si Mwenyekiti au Katibu. Hapa mimi siandiki maneneo haya kukufanya udhani kuwa nataka kuwa king’ang’anizi kwenye wadhifa niliovuliwa, la hasha bali napenda upate picha halilisi ya uendeshwaji wa Siasa ya CHADEMA na kisha uweze kugundua uhalisia wa mgogoro ulivyo. Viongozi wa CHADEMA Makao Makuu wamening’oa kutoka katika wadhifa niliokuwa nao kwa sababu zao binafsi na si sababu za chama kama chama, na wanajitahidi kuzunguka mikoani kwa siri kuendelea kunichafua kisiasa kuwa sifai. Kweli sifai kwa wafuja ruzuku ya chama, kweli sifai kwa mafisadi ndani ya chama ila nafaa kukiendesha chama katika ngazi ya taifa katika nafasi yoyote na siku zote. Nafaa kwa sababu nimefukuzwa kwa kusema ukweli hivyo nikageuka mwiba kati kati ya majipu, nikatolewa. Ndiyo, nafaa kwa sababu siko tayari kufanya kazi na watu waliozoea kukaa ofisini kama mafaili! Nafaa kwa sababu mimi ni mpambanaji, kamanda shujaa niliye tayari kuwajibishwa kwa ajili ya kuwatetea WANADEMOKRASIA hususan WANACHADEMA nchi nzima.

Kuliendesha Taifa kama Tanzania hakuhitaji siasa za kisanii, fitina, na chuki. Kinachotakiwa ni nani abadilike alete mabadiliko katika siasa ili aweze kukabidhiwa dola na alete mabadiliko. Wananchi wamechoshwa na siasa zetu ndio maana wanaziita siasa za kisanii. Wanahitaji mabadiliko. CHADEMA maana yake ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo, lakini huku wanakoelekea tayari uongozi wa Mbowe na Slaa wameiondosha Demokrasia kwa kunitoa katika wadhifa wa umakamu Mwenyekiti kwa kupiga kampeni ndogo ya wajumbe 31 tu! Tena huku wakinituhumu kuwa navujisha siri za chama!!. Dhahama kama hii siwezi kuivumilia hata kidogo na ni wazi kuwa hata wanachama wetu hawajafurahishwa na jambo hili. Mimi nilipokuwa kwenye ngazi hiyo ndipo fedha zilipoanza kupelekwa mikoani kwa viwango halali, ndipo ukarabati wa Makao Makuu ulifanyika. Niweke wazi hapa kuwa, jambo lililonifanya niandike jarida hili si kuwashawishi Freeman Mbowe na Slaa kunirudisha kwenye nafasi waliyonitoa kwa matusi, la hasha! Lengo ni kuweka wazi kwa wanachama wajue aina ya uongozi uliopo Makao Makuu ya Chama. Kama ni suala la mimi kurudi katika nafasi hiyo ni mimi mwenyewe nikiamua na kwa kutumia Demokrasia. Ikumbukwe kuwa, Freeman ndiye aliyesema kuwa hataki kufanya kazi na mimi na kutokana na UMANGIMEZA na Kauli za NDIYO MZEE akapata kuungwa mkono na wajumbe 31 tu! Baada tu ya mimi kutangazwa kuwa nimetolewa kwenye wadhifa niliokuwa nao nilipata simu nyingi sana za wanachama na hata baadhi ya watendaji Makao Makuu wakiniambia kuwa kama Mbowe hayuko tayari kufanya kazi na mimi, wao bado wananihitaji katika Uongozi Taifa. Kuna mila ya kichagga kuwa, katika eneo la kazi/biashara, ukimuona anayekusababisha ukose maslahi Fulani unatakiwa kumuondoa kwa gharama yoyote! Na hili ndilo lililojiri kwangu na mwenyekiti wangu.

Aluta Continue…………………..

Wangwe Chacha Zakayo,
Mbunge wa Tarime-CHADEMA


KAULI YANGU KWA MSOMAJI

Awali ya yote, nasikitika sana kwa maamuzi yaliyofikiwa na wajumbe 31 kule Dodoma aidha, kwa hasira, chuki au majungu na kuamua kuniondoa katika wadhifa niliokuwa nao wa Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara wakitumia kivuli cha Katiba ya Chama. Pili nimezidi kuumia zaidi pale nilipotuhumiwa kuwa eti navujisha siri za Chama kwa CCM! Niliwapa siku Arobaini (40) kuwaza kuthibitisha juu ya tuhuma hizo lakini wameshindwa hadi leo! Inamaanisha kuwa walitumia tuhuma hizo ili kunitoa kati yao ili nisiendelee kutetea ahadi za wanachama wa CHADEMA na nisiendelee kupinga ubadhirifu wa fedha za chama. Pengine kutokana na hasira, chuki na majungu hayo hayo wakaamua kuzidi kunichafualia jina katika mkutano uliofanyika Tanga kwa kunisema kuwa mimi ni mhuni. Hapa sintakuwa na huruma wala urafiki na yeyote aliye mstari wa mbele kunichafua kisiasa nitahakikisha nawafungulia mashtaka na waweze kuthibitisha tuhuma hizo. Mpendwa msomaji, pamoja na hayo ni vyema ukumbuke kuwa, uongozi wa CHADEMA Taifa umeshindwa kukieneza chama hadi vijijini. Ni kwa ajili ya majungu haya haya!.

Kimsingi, tusiposhikamana kwa sauti moja, lengo moja na kwa msimamo, ni dhahiri kuwa chama cha mapinduzi kitaendelea kushika Dola hadi Ukamilifu wa Dahari! Chama kisipokuwa madhubuti hakitaweza kushika Dola hakiwezi kuaminika na Wananchi. CHADEMA tufike mahali tugeuke, tujue tuna lengo la kuiongoza Tanzania na si vinginevyo. Badala ya kulewa katika kuwafichua mafisadi. Tumejisahau!.

Naamini kuwa, nguvu za umma ndiyo nguvu inayoweza kuleta mabadiliko ya kweli.

Naamini kuwa, katika chama chochote cha siasa, mwanachama ndiye bora kuliko Kiongozi.

Naamini kuwa msingi bora wa chama hujengwa na watu makini.

Naamini pia baada ya kusoma Jarida hili ukiwa kama mwanachama au Mwanademokrasia utaungana nami katika kupiga vita UFISADI ndani ya CHADEMA.

4 comments:

Anonymous said...

Waoooh! I cant believe this story but its true... hawa kina mbowe hawana lolote sasa ndio naamini wamemchifupa chacha wa watu, hawataki kuambiwa ukweli jamani viongozi gani hawa kazi kuwaona na kiwasema wenzao wa ccm oohoo mafisadi kumbe wao ndio nmba 1 WAMEVAA NGOZI YA KONDOO KUMBE MASIMBA LOH! Poleni familia ya chacha mungu awape subira ktk kipindi hiki kigumu.R.I.P chacha

Anonymous said...

DAYYM! Ndio maana alikolimbwa Chacha wa watu!

Anonymous said...

lakini ni vyema tuelezwe na upande mwingine wa shilingi,ili tuwatendee haki CHADEMA kwani Chacha wangwe si malaika na tukubali kila kitu alichosema/kundika!
mbona hatuelezwi juu ya mikakati yake ya kuisambaratisha CHADEMA na kisha kurudi CCM?

VIKAO VYA SIRI NA WATU WALIOSIMAMISHWA UONDZI KATIKA CHAMA KWA UTOVU WA NIDHAMU KWA KIONGOZI WA HADHI YAKE YA UMAKAMU MWENYEKITI VYA NINI?KWANINI ASIWAHIITE OFISINI WAZUNGUMZE KAMA SIYO HILA NA FITNA?

na hataki CHADEMA ilipe madeni yanayoyokana na kampeni ikiwa ni pamoja na kukodisha helikopta...lakini anafurahi chadema kupata ruzuku ya milioni 60 kwa mwezi bila kujiuliza zimepatikana vipi kama si kamapeni na mikakati ya gharama kama vile kukodisha helikopta au anadhani helikopta ni mali ya CHADEMA,MBOWE au SLAA?
ukaribu wake na Dr.walibu kaburou ulikuwa unamaslahi gani kwa CHADEMA?

UKARIBU WAKE YEYE NA MAKAMBA ULIKUWA UNA MASLAHI GANI KWA CHADEMA?
KWENYE MAKALA YAKE ANAONESHA KUWA ZINAPOTOKEA FURSA ZA KWENDA NJE KWA VIJANA WANAKWENDA WA MAKAO MAKUU TU ANATAKA NA WA TARIME WAENDE HUU NI UMBUMBU KWA VIONGOZI HAMUWEZI KWENDA WOTE.....SUALA NI UWAKILISHI NA NDIYO MAANA HATA YEYE CHACHA WANGWE ALIKUWA ANAWAWAKILISHA BUNGENI...NA SI WATARIME WOTE WAENDE BUNGENI!

KIMSINGI MIMI SI MWANACHAMA WA CHADEMA INGAWA NA FUATILIA SANA SIASA ZA VYAMA VINGI...KWA JINSI NILIKUWA NA MCHUKULIA MAREHEMU MHE.CHACHA WANGWE ....SI MWANASIASA MAKINI NA ALIKUWA NI MTU WA KUKURUPUKA NA JAZBA NYINGI,PUPA/PAPARA...NDIYO MAANA ALISHINDWA KUTULIA NA KUFANYAKAZI KAMA MAKAMU MWENYEKITI NA NDANI YA KIPINDI KISICHOZIDI MIEZI 6 AKAANZA KUTAKA UWENYEKITI.....KWA MWANASIASA MAKINI UWEZI KUKURUPUKIA MADARA NAMNA HII....NADHANI HATA SHULE ILIKUWA KIKWAZO KIKUBWA SANA KWAKE KAKTIKA KUPAMBANUA MAMBO MAZITO..KWANI HATA KANUNI PALE BUNGENI KWA KIPINDI CHA MIAKA MIWILI ALIZOKAA BUNGENI BADO ZILIKUWA NI MZIGO MZITO SANA KWAKE!

Anonymous said...

mbowe fisadi number moja,na mungu anaanza kuwaipa hapa hapa duniani,kwanza kafukuzwa msibani na cha pili wanaikosea jimbo la tarime,wanachukua nccr au ccm,kwa hiyo ruzuku pia kwao ndo inazidi kupungua.hamna rangi wataacha kuona.hawa na mtikila hakuna tofauti,hawajui siasa waa sio wanasiasa.mchangiaji wa tatu anasema shule ilikuwa kikwazo cha marehemu wangwe,amesahau kuwa mbowe yenyewe yana shule,kafeli form 6,juzi kajaribu kusoma kumemshinda karudi bongo kugombania ruuku.chadema si chama bal ini NGOS