Monday, August 18, 2008

Taarifa ya Ikulu - EPA

Taarifa ya Ikulu kuhusu EPA


DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
UNITED REPUBLIC OF TANZANIA

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
E-mail : press@ikulu.go.tz
Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,THE STATE HOUSE,
P.O. BOX 9120
DAR ES SALAAM.Tanzania.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo (Jumatatu, Agosti 18, 2008) amepokea rasmi ripoti ya uchunguzi wa upotevu wa fedha za Akaunti ya Malipo ya Nje (External Payments Accounts - EPA) katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Rais Kikwete amekabidhiwa ripoti hiyo na Mwenyekiti wa Timu iliyokuwa inafanya uchunguzi huo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson P.M. Mwanyika.Mwanasheria Mkuu huyo alifuatana na wajumbe wengine wa Timu hiyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Edward Hosea.

Rais amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wa Timu hiyo kwa kazi kubwa na ngumu lakini nzuri.Rais, baada ya kuwa ameisoma na kuitafakari ripoti hiyo, ataitolea maamuzi katika siku chache zijazo, na taarifa rasmi ya maamuzi hayo ya Rais itatolewa kwa wananchi.

Timu hiyo iliundwa na Rais Kikwete Januari 9, mwaka huu, 2008 katika tangazo rasmi lililotolewa kwa waandishi wa habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo.Wakati anaunda Timu hiyo, Rais aliipa muda wa miezi sita kukamilisha kazi yake, ambayo ilikuwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa fedha zilizolipwa isivyo halali zinarudishwa.

Rais aliunda Timu hiyo baada ya kuwa amepitia Taarifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Mwaka wa Fedha 2005/06 za EPA katika Benki Kuu Tanzania (BOT), uliofanywa na Wakaguzi wa Kampuni ya Ernst and Young, kwa niaba ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.Kampuni hiyo ya Ernst and Young iliombwa na Serikali kuifanya kazi hiyo.

Iliianza Septemba, 2007 na kumalizika Desemba, mwaka huo huo, 2007. Rais Kikwete alikabidhiwa Taarifa hiyo Januari 7, mwaka huu, 2008 na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali. Siku ya tatu, baada ya kuwa ameisoma na kuifanyia kazi, Rais aliitolea maamuzi Taarifa hiyo, ikiwa ni pamoja na kuunda Timu ya Mwanyika.

Imetolewa naKurugenzi ya Mawasilia ya Rais,

Ikulu,DAR ES SALAAM.

18 Agosti, 2008

2 comments:

Anonymous said...

Pamoja na habari hizo za kutuka nyumbani, kuna habari kwamba Rais wa Zambia amefariki hospitalini huko Ufaransa!

Anonymous said...

Hadidu za rejea hazikusema timu iandike ripoti bali iwachukulie hatua za kisheria watakaobainika kuhusika na wizi wa pesa za EPA. Sasa haya ya kuandika ripoti yametokea wapi? Labda kama ripoti inazungumzia hatua zilizochukuliwa kwa wahusika - kitu ambacho sidhani kimefanyika - inaelekea hata huyo aliyetoa 'tenda' hiyo (JK) ama hajui anachofanya au anaendeleza 'usanii'.