Tuesday, April 15, 2008

Choo Chako


CHOO CHAKO NI KIPIMO HALISI CHA AFYA YAKO


Kabla hujapatwa na matatizo makubwa ya kiafya, kuna dalili ambazo hujionesha wakati unapokwenda kujisaidia haja kubwa ama ndogo, dalili ambazo mara nyingi huzijui kuwa ni kiashiria kwamba una tatizo la kiafya.


Katika makala ya leo, tutaangalia aina kadhaa za choo ambazo huashiria kuwa unaupungufu wa aina moja au zaidi ya chakula fulani, au mwili wako unahitaji aina moja au zaidi ya chakula ili kuleta uwiano katika mwili wako.Labla kabla sijaanza moja kwa moja kutaja aina hizo za choo (haja kubwa), ningependa kutoa dokezo moja kuhusu dalili zinazojionesha wakati tunapojisaidia haja ndogo, lakini tunashindwa kutambua ni dalili ya kitu gani. Haja ndogo ya rangi ya njano au kahawia, huashiria upungufu wa maji mwilini, hivyo kunywa maji ya kutosha, hata kama husikii kiwi. Hakikisha siku zote mkojo wako ni mweupe.


1. CHOO KIGUMU CHENYE UMBO MFANO WA KARANGA


Unapotoa choo cha aina hii, ni dalili kwamba una upungufu wa vyakula vyenye ‘faiba’ (ufumwele), huna maji ya kutosha na usagajwi wa chakula tumboni ni wa taratibu. Suluhisho ni kuongeza kiasi cha maji unachokunywa, kunywa chai ya viungo (herbal tea), matunda na mboga mboga kwa wingi.Vile vile ongeza ulaji wa vyakula vya nafaka, kama vile wali, (brown rice), ugali wa mtama na ulezi. Epuka ulaji wa nyama, mayai, ngano, sukari na bidhaa zitokanazo na maziwa.


2. CHOO UMBO LA ‘SOSEJI’ LAKINI YENYE VIGOLOLI


Aina hii ya choo inaashiria kwamba choo kimekaa muda mrefu sana kwenye utumbo mkubwa. Maji mengi na chakula chenye faiba ya kutosha, kama maharage, wali, ugali vinahitajika. kama ilivyoelezwa hapo juu, ongeza kiwango cha maji unachokunywa, kula matunda na mboga, pia epuka kula vyakula vyenye wanga na sukari nyingi.


3. CHOO MFANO WA ‘SOSEJI’ LAKINI YENYE NYUFA


Choo cha aina hii si dalili ya kitu kingine bali ni upungufu wa maji mwilini, hivyo kunywa maji mengi kwa siku. Kutegemeana na kazi unazozifanya, lakini kiwango cha chini cha maji unachopaswa kunywa kwa siku, ni lita moja na nusu.


4. CHOO MFANO WA ‘SOSEJI’ LAKINI LAINI NA HAKINA NYUFA


Ukitoa choo cha aina hii, ambacho hata wakati wa kujisaidia kinatoka taratibu, jipongeze, kwani ni dalili kuwa uwiano wa vyakula unavyokula na maji uko sawa. Hongera!


5. CHOO CHA MABONGE YENYE NCHA, KINACHOTOKA KIRAHISI


Hii inaweza kuwa dalili kwamba chakula kinasagwa haraka sana tumboni, hali hii inaweza kusababisha ukosefu wa virutubisho na maji mwilini. Ongeza mlo wako wenye ‘faiba’ ya kutosha, hasa kula wali, ugali wa mtama, ulezi na hata virutubisho vingine unavyoweza kuvipata kwa njia ya vidonge (food supplements)


6. CHOO CHA VIPANDEVIPANDE NA LAINI MFANO WA UYOGA


Halikadhalika choo cha aina hii kinaashiria kuwa hakuna maji ya kutosha mwilini, usagaji wa chakula ni wa haraka sana na kuna unyonyaji duni wa virutubisho. Hali hii inasababishwa na mlo duni au mwili kukataa baadhi ya vyakula. Kula vyakula vyenye ‘faiba’ ya kutosha kama ilivyoelezwa hapo juu, acha kula matunda, juisi na mboga kwa muda.


7. CHOO CHA MAJIMAJI MATUPU


Choo cha aina hii siyo kizuri, mara nyingi kinaashiria uambukizo wa ugonjwa fulani. Nenda hospitali kafanyiwe uchunguzi wa kiafya. Kula vizuri, hasa vyakula vya nafaka, supu halisi ya mbogamboga ili kurejesha virutubisho vilivyopotea kutokana na kuharisha. Hakikisha unarejesha maji yaliyopotea mwilini kwa kunywa maji ya kutosha na chai ya viungo (herbal tea).



Uchambuzi huu wa choo, umefanywa hivi karibuni na Dk. K. W. Heaton, ambaye ni msomaji wa tiba katika Chuo Kikuu cha Bristol, Uingereza.


6 comments:

Anonymous said...

Doh! Wacha nikimibilie hospitali nikapime choo!

Simon Kitururu said...

Ukiwa unatumia choo hicho hapo pichani(cha shimo), ni vigumu kweli kustukia karanga, nyufa,nk., kwenye soseji. Labda hicho cha majimaji!DUH!

Anonymous said...

Leo naona umeamua kuongea mavi matupu.

Anonymous said...

Kwa kweli hii somo ni muhimu. Tunacheka na kudharau lakini kila mtu anaenda haja.

Anonymous said...

Ni kweli tunakunyaga bila kufikiria hayo makimba yakoje. Sasa nitakuwa natazama kila nikinya!

Anonymous said...

mh!! Kama ndivyo mie nahitajika kunywa simtank ya lita 50 kila siku. Mwe!! ahsante kwa hili somo wengine limetufumbua macho ati!!! Haika.